Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya (KCCB) limepiga marufuku hotuba zote za kisiasa katika makanisa ya Kanisa Katoliki kote nchini humo, wakati taifa likijiandaa kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka 2027.
Kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa Novemba 13, 2026 na Vatican News, tamko hilo lililotolewa mjini Embu na kusainiwa na Mwenyekiti wa KCCB, Askofu Mkuu Maurice Muhatia Makumba wa Jimbo Kuu la Kisumu, limeelekeza mapadre wote kuhakikisha nyumba za ibada zinabaki kuwa maeneo ya sala, umoja, na ukarimu kwa waumini wote bila kujali itikadi zao za kisiasa.
“Watu kutoka katika makundi mbalimbali ya maisha huja katika nyumba za ibada kutafuta amani na kuwa kimya mbele ya Yesu. Kipindi cha kampeni za uchaguzi hakipaswi kuwa sababu ya kufanya nyumba za ibada kuwa majukwaa ya kisiasa,” wamesema Maaskofu, wakisisitiza kuwa wanasiasa wana majukwaa mengine kama vile mikutano ya hadhara na vyombo vya habari.
Tamko hilo lenye kaulimbiu “Wito wa Kuijenga Kenya Yenye Haki, Amani na Umoja”, limeongozwa na maandiko kutoka Mika 6:8 pamoja na rejea ya Waraka wa Kitume wa Papa Leo XIV (Magnifica humanitas), likikumbusha wajibu wa Kanisa kusimama upande wa wanyonge pale utu wa binadamu unapokiukwa.
Maaskofu hao wamewapelekea vijana ujumbe maalumu wakiwataka kuchukua hatua za kiuwajibikaji kwa kupata vitambulisho vya kitaifa na kujiandikisha kupiga kura. Hata hivyo, wamewaonya vikali dhidi ya kutumiwa na wanasiasa kuchochea vurugu kwa ushawishi wa fedha. Wamewahimiza vijana kuwa vielelezo vyema katika jamii na kutumia ubunifu wao kwenye mitandao ya kijamii kueneza amani, haki, na utunzaji wa mazingira badala ya chuki na migawanyiko.
Kuelekea uchaguzi wa 2027, KCCB iMEtaka Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kujenga imani kwa wananchi kwa kuhakikisha mchakato mzima kuanzia usajili wa wapiga kura hadi utangazaji wa matokeo unakuwa huru, wa wazi, na usioingiliwa na wenye mamlaka. Aidha, wameitaka Mahakama kutenda haki bila upendeleo katika migogoro yote ya uchaguzi.
Wakigeukia Bunge la Kitaifa, Maaskofu wameonya dhidi ya kupitisha sheria zinazoweza kufifisha imani ya wananchi, wakipinga vikali mapendekezo ya kuzuia matangazo ya moja kwa moja (live broadcast) ya kuhesabiwa kwa kura za urais. Pia, wameeleza wasiwasi wao kuhusu miswada sita ya elimu iliyo bungeni, wakidai baadhi ya vifungu vyake vinakiuka misingi ya ushirikishwaji na vinaweza kudhoofisha taasisi za elimu zilizoanzishwa na mashirika ya dini.
Katika eneo la ulinzi na usalama, KCCB imeeleza kusikitishwa na kuendelea kwa matukio ya utekaji nyara, watu kupotea katika mazingira ya kutatanisha, na unyanyasaji wa watetezi wa haki za binadamu baadhi ya matukio yakidaiwa kuhusisha watu wenye silaha wanaoshirikiana na vyombo vya dola. Maaskofu wamevitaka vyombo vya usalama kutekeleza sheria kwa usawa bila upendeleo, huku wakiwaasa wananchi kutumia uhuru wao wa kujieleza bila kutoa kauli za ukabila au uchochezi.