Jeshi la Polisi Kikosi cha Wanamaji Tanzania limezindua kampeni ya Ongea na Kamanda katika Soko la Samaki Feri, Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam, Oktoba 12, 2026, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha ushirikiano kati ya polisi na wananchi pamoja na kusikiliza changamoto zinazowakabili.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Kamanda wa Kikosi cha Polisi Wanamaji Tanzania, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi Moshi N. Sokoro, amewataka wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya athari zinazoweza kusababishwa na mvua za El Niño, huku akisisitiza umuhimu wa kuchukua hatua za kujikinga na majanga yanayoweza kujitokeza.

Sokoro pia amewataka wananchi wanaomiliki silaha kinyume cha sheria kuzisalimisha kwa mamlaka husika, akieleza kuwa umiliki wa silaha bila kufuata sheria, taratibu na kanuni zilizowekwa unaweza kuhatarisha usalama wa watu na jamii kwa ujumla.
Amesema ushirikiano kati ya wananchi na Jeshi la Polisi ni muhimu katika kujenga jamii yenye amani, upendo, mshikamano na matumaini, huku akiwahimiza wananchi kutumia kampeni ya Ongea na Kamanda kuwasilisha kero, maoni na changamoto zinazohitaji ufumbuzi.
Aidha, amewataka wavuvi kuendeleza ushirikiano katika shughuli zao za kila siku ili kuimarisha mshikamano na kuhakikisha usalama wao wanapokuwa baharini.
Kwa upande wake, Meneja wa Soko la Samaki Feri, Selemani Abdalah Mfinanga, amelishukuru Jeshi la Polisi kwa kuifikisha kampeni hiyo sokoni, akisema ni fursa muhimu ya kusikiliza kero, maoni na hoja za wananchi kwa lengo la kujenga jamii bora.
Mfinanga ameahidi kuwa changamoto zilizowasilishwa zitafanyiwa kazi, akisisitiza umuhimu wa kushirikiana na wadau husika ili kutafuta ufumbuzi wa matatizo yanayowakabili wafanyabiashara na wavuvi katika soko hilo.
Katika mkutano huo, wavuvi wamewasilisha changamoto mbalimbali zinazohitaji kushughulikiwa ili kuboresha usalama na mazingira ya kazi zao.
Miongoni mwa changamoto hizo ni hitaji la kupatiwa boti ya uokoaji itakayosaidia wakati wa dharura baharini, pamoja na kupewa elimu kuhusu matumizi sahihi ya makoti ya kujiokoa (life jackets) na vifaa vya kuzimia moto (fire extinguishers).
Wavuvi hao pia wameomba kuimarishwa kwa ushirikiano kati ya viongozi na wavuvi panapotokea majanga baharini, huku wakitaka hatua zichukuliwe kuzuia wavuvi wakubwa kuwaonea wavuvi wadogo katika shughuli zao za kiuchumi.
Vilevile, wameiomba mamlaka husika kufanya marekebisho ya maeneo ya kukaa na miundombinu ya soko, wakieleza kuwa baadhi ya mabati yamechakaa na yanahitaji kubadilishwa kabla ya kuanza kwa mvua za El Niño ili kuimarisha usalama na mazingira ya kazi.
Kampeni ya Ongea na Kamanda inalenga kutoa nafasi kwa wananchi kuwasilisha changamoto zao moja kwa moja kwa viongozi wa Jeshi la Polisi, kuimarisha mawasiliano na kujenga ushirikiano katika kudumisha amani na usalama nchini.