Mkurugenzi wa Taasisi isiyo ya Kiserikali ya Lebao’s Kids Foundation (BKF), Theophil Muyinga, ameiomba Serikali kutoa kipaumbele katika upatikanaji wa bima ya afya kwa wote, hususan kwa makundi maalumu, yakiwemo watoto wenye ulemavu na yatima kutoka familia zenye hali duni ya kiuchumi.
Muyinga ametoa ombi hilo wakati wa zoezi la kugawa bima za afya kwa watoto wenye ulemavu wanaohudumiwa na kituo cha Lebao’s Kids Foundation (BKF) pamoja na watoto yatima kutoka kituo cha kulelea watoto yatima kilichopo Migoli Mkoani Iringa, ziezi lililoandaliwa na taasisi hiyo kwa ushirikiano na mfuko wa Bima ya Afya ya Jamii (CHF).

Amesema familia nyingi wanazotoka watoto hao zinakabiliwa na changamoto za kiuchumi, hali inayozifanya kushindwa kumudu gharama za matibabu, hivyo kusisitiza umuhimu wa Serikali kuhakikisha makundi hayo yanapata kipaumbele katika mipango ya bima ya afya.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mwenza wa taasisi hiyo, Catherine Moreno, naye amechangia hoja hiyo, akisisitiza umuhimu wa kuimarisha juhudi za kusaidia watoto wenye uhitaji ili waweze kupata huduma za afya zinazostahili.
Akijibu hoja hiyo, Afisa Uandikishaji wa Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) katika Manispaa ya Iringa, Kokwiliza Katemana, amesema jukumu la Serikali ni kulinda afya za wananchi wake, huku watoto wakiwa miongoni mwa makundi muhimu yanayohitaji kupewa kipaumbele katika upatikanaji wa huduma za afya.
Katemana amesema katika awamu hii, Serikali imeweka mkazo katika kuwafikia watu wa makundi maalumu pamoja na kaya zisizo na uwezo wa kiuchumi, ili nao waweze kunufaika na huduma za bima ya afya.

Utoaji wa bima hizo unalenga kupunguza mzigo wa gharama za matibabu kwa watoto hao na familia zao, pamoja na kuwawezesha kupata huduma za afya wanapokabiliwa na changamoto za kiafya.
Hatua hiyo inakuja wakati Serikali ikiendelea na utekelezaji wa awamu ya pili ya mpango wa Bima ya Afya kwa Wote, unaolenga kupanua wigo wa upatikanaji wa huduma za afya na kupunguza gharama zinazobebwa na wananchi wanapougua.