Latest Posts

CHADEMA YADAI LISSU AMEANZA MGOMO WA KULA, MAGEREZA YAKANUSHA

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimedai kuwa Mwenyekiti wake, Tundu Lissu, ameanza mgomo wa kula chakula kuanzia tarehe 26 Oktoba 2026 akiwa gerezani, huku mawakili wake watatu wakizuiwa kuingia gerezani kumuona

Kwa mujibu wa taarifa rasmi iliyotolewa Oktoba 26, 2026 na Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa CHADEMA, Brenda Rupia, chama hicho kilitangaza kuwa Lissu alifikia uamuzi wa kuanza mgomo wa kula kutokana na wasiwasi juu ya upatikanaji wa haki yake ya msaada wa kisheria na mawasiliano na mawakili wake.

Rupia ameeleza kuwa mawakili watatu wa Lissu, Dickson Matata, Doris Kafuku na Neema Massame walikwenda gerezani tarehe 26 Oktoba 2026 kwa lengo la kumuona na kuwasiliana naye, lakini walizuiwa kuingia ndani na mamlaka za gereza

“Leo, mawakili wake watatu, Dickson Matata, Doris Kafuku na Neema Massame, walikwenda gerezani kwa lengo la kumuona na kuwasiliana naye, lakini walizuiwa kuingia. CHADEMA inaeleza wasiwasi wake mkubwa kuhusu kuzuiwa kwa mawakili hao kumwona Mwenyekiti wa Chama, hasa wakati huu ambapo tayari ameanza mgomo wa kula. Hali hii inazua maswali mazito kuhusu kupatikanaji wa huduma za kisheria na namna haki za Mheshimiwa Tundu Lissu zinavyolindwa akiwa gerezani”, ameeleza Rupia.

CHADEMA imezitaka mamlaka husika kuhakikisha mawakili hao wanaruhusiwa kumwona Lissu bila vikwazo visivyo na msingi wa kisheria na kuchukua hatua za haraka kulinda usalama na ustawi wake

Akijibu madai hayo kupitia taarifa kwa umma iliyotolewa Oktoba 27, 2026, Msemaji wa Jeshi la Magereza, SACP Elizabeth Mbezi ameeleza kuwa taarifa zilizosambazwa na CHADEMA si za kweli, ni za upotoshaji na zinalenga kuleta taharuki katika jamii.

Amefafanua kuwa mahabusu Tundu Lissu yupo salama gerezani na wala hayupo kwenye mgomo wa kula chakula kama ilivyoripotiwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano wa CHADEMA.

Kuhusu suala la mawakili, SACP Mbezi amebainisha kuwa mawakili wanaomwakilisha Lissu wameendelea kuruhusiwa kuonana na mteja wao kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizopo mara baada ya kujiridhisha kuwa ni mawakili wake halali

“Jeshi la Magereza linapenda kuujulisha umma kwamba, Mahabusu Tundu Lissu yupo salama na hayupo katika mgomo wa kula chakula kama ilivyorotiwa. Kuhusu kutembelewa na mawakili wanaomwakilisha wameendelea kuruhusiwa kuonana na mteja wao kwa mujibu wa taratibu baada ya kujiridhisha kuwa ni mawakili wake na si vinginevyo. Jambo hili limekuwa likitekelezwa kwa mujibu wa Sheria na Taratibu zilizopo”, imeeleza taarifa hiyo.

SACP Mbezi ameongeza kuwa katika kutekeleza majukumu yake ya kuwapokea, kuwahifadhi na kuwarekebisha wanaoshikiliwa, Jeshi hilo limekuwa likizingatia usalama, sheria, kanuni, utu na misingi ya haki za binadamu. Amewataka wananchi kupuuza taarifa hizo zisizo na ukweli na kuacha kuzisambaza kwani kufanya hivyo ni kosa kisheria.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!