Chimbo la Vijana limeendelea kuwa daraja muhimu la kuwaunganisha vijana na Serikali pamoja na taasisi mbalimbali zinazotoa huduma za uwezeshaji wa mitaji na fursa za kiuchumi, kwa lengo la kuwainua vijana kiuchumi na kuwasaidia kutatua changamoto zinazowakabili.
Akizungumza na waandishi wa habari mapema leo, Mkuu wa Wilaya ya Geita, Hashim Komba, amesema Novemba 21 mwaka huu vijana wa Wilaya ya Geita watapata fursa ya kukutana na Serikali pamoja na taasisi mbalimbali zinazotoa huduma na fursa za kiuchumi, katika jukwaa linalolenga kufungua milango ya maendeleo kwa vijana.

Komba amesema Serikali inatambua kuwa vijana wana mawazo, maoni na ubunifu mwingi unaoweza kuchochea maendeleo, hivyo ni muhimu kuwapa nafasi ya kueleza changamoto zao na kuwasilisha mapendekezo yao ili kwa pamoja waweze kushiriki katika kujenga wilaya yao na taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake, Mratibu wa Chimbo la Vijana Branch 2026, Scholastical Mchopanga, amesema jukwaa hilo limeandaliwa kwa lengo la kuzikutanisha sekta na taasisi mbalimbali na vijana ili kuwafikishia huduma, fursa na taarifa muhimu zinazoweza kuwasaidia kujikwamua kiuchumi.
Baadhi ya vijana wameeleza kufurahishwa na uwepo wa jukwaa hilo mkoani Geita, wakisema litawapa fursa ya kukutana na wadau mbalimbali, kupata elimu na kufahamu fursa zinazoweza kuwasaidia katika shughuli zao za kiuchumi na maendeleo yao kwa ujumla.