Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linamshikilia na kumhoji kwa kina Peter Mmasi (32), mkazi wa Kimara, kwa tuhuma za kumzuia na kumshambulia askari polisi aliyekuwa akitekeleza wajibu wa kisheria wa kumkamata.
Tukio hilo limebainishwa kupitia taarifa rasmi kwa umma iliyotolewa leo, Novemba 11, 2026 na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, SACP Jumanne Muliro.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya Polisi, askari aliyefanyiwa shambulio hilo ni Sajenti Johnson Sylivery, ambaye alikuwa katika jitihada za kumkamata mtuhumiwa huyo kufuatia tuhuma za kutishia kumuua raia. Mwananchi aliyetishiwa kuuawa na mtuhumiwa huyo ametajwa kuwa ni Carisma Amedeus Kileo, ambaye pia ni mkazi wa Kimara jijini Dar es Salaam.
Jeshi la Polisi limeeleza kuwa taratibu zote za kisheria zinaendelea kukamilishwa dhidi ya mtuhumiwa huyo.