Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametoa wito wa kuongeza juhudi za kuhakikisha kila kaya barani Afrika inapata nishati safi ya kupikia, akisisitiza kuwa mafanikio ya ajenda hiyo yanapaswa kupimwa kwa idadi ya familia zinazopata huduma hiyo kwa gharama nafuu na endelevu.
Akizungumza katika mkutano wa ngazi ya juu kuhusu nishati safi ya kupikia barani Afrika, uliofanyika pembezoni mwa Mkutano wa 31 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP31), jijini Antalya, Uturuki, Novemba 12, 2026, Rais Samia amesema licha ya hatua zilizopigwa, takribani watu bilioni moja barani Afrika bado hawana huduma ya nishati safi ya kupikia.

Amesema hali hiyo inachangia vifo vya takribani watu 850,000 kila mwaka, huku wanawake na watoto wakiendelea kuathiriwa na moshi unaotokana na matumizi ya nishati zisizo safi pamoja na muda mwingi wanaotumia kutafuta kuni.
Rais Samia amesema matumizi ya kuni na nishati nyingine za jadi pia yanaongeza ukataji wa misitu, uharibifu wa mazingira na uzalishaji wa gesi chafuzi, hivyo kuna umuhimu wa kuongeza kasi ya upatikanaji wa teknolojia safi za kupikia.

Ameeleza kuwa mkutano wa kilele kuhusu nishati safi ya kupikia uliofanyika Paris mwaka 2024 ulihamasisha ahadi za kifedha za dola bilioni 2.2, huku juhudi zilizofuata zikiongeza ahadi hizo kufikia takribani dola bilioni 3.1.
Amehimiza nchi za Afrika, washirika wa maendeleo na sekta binafsi kuimarisha ushirikiano ili rasilimali zinazokusanywa zigeuke kuwa suluhisho halisi kwa wananchi.