Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba amewataka wadau wa elimu wajadili namna ya kuimarisha upatikanaji wa mapato ya ndani ambayo yataboresha uwezo wa nchi kutekeleza vipaumbele vya kitaifa.
Amesema kwenye suala la elimu, upatikanaji wa fedha unapaswa kuwa endelevu na unaoambatana na mipango ya uhakika, utoaji wa fedha kwa wakati, manunuzi sahihi, uwazi kwenye matumizi ya fedha na matokeo yanayoweza kupimika

Ametoa wito huo leo (Alhamisi, Novemba 12, 2026) wakati akifungua Mkutano wa Sita wa Kimataifa wa Ubora wa Elimu katika ukumbi wa JNICC, jijini Dar es Salaam.
Waziri Mkuu amesema katika kupanga matumizi ya fedha zinazopelekwa kwenye sekta ya elimu, hawapaswi kuangalia tu mgao wa fedha hizo, bali wahoji endapo zinafika kwenye shule zilikopangiwa na zinatumiwa na wanafunzi wanaozihitaji zaidi.
“Lazima tuimarishe utekelezaji wa bajeti zinazopelekwa, tupunguze uzembe, tuboreshe uratibu baina ya taasisi za kitaifa na za kwenye maeneo yetu na tutumie takwimu za kuaminika katika kufanya maamuzi. Kila shilingi iliyowekezwa kwenye elimu inapaswa kuchangia ufundishaji bora, matokeo bora na fursa za sawa,” amesema.

Amesema wanajadili suala upatikanaji wa fedha na ubora wa elimu, maamuzi yatakayofikiwa yanapaswa kuzingatia usawa na ujumuishi kwa wanafunzi. “Rasilimali zitakazopatikana zinapaswa kujibu mahitaji ya wanafunzi wa kike, wanafunzi wenye mahitaji maalum ya elimu, watoto walioathiriwa na umaskini, wale walio katika jamii ambazo hazijahudumiwa na wanafunzi wote wanaokabiliwa na vizuizi vya kielimu.”
“Hakuna mtoto anapaswa kuachwa kwenye mfumo wa elimu yetu kwa sababu ya mahali anapoishi au mazingira yanayomzunguka. Tunapaswa tuhakikishe kuwa shule ziko salama, zinafikika na zina mazingira ambayo kila mwanafunzi anaweza kushiriki.”
Akielezea kuhusu maandalizi ya mfumo wa kupokea makundi mawili ya wahitimu ifikapo mwaka 2028 kutokana na mabadiliko ya mfumo wa elimu kupitia Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014, Toleo la 2023, pamoja na mitaala iliyoboreshwa, Waziri Mkuu amesema kipindi hiki cha mpito kinahitaji maandalizi yaliyoratibiwa baina ya taasisi za Serikali na wadau wa elimu.
Waziri Mkuu amesema lengo la mabadiliko hayo ni kuongeza elimu ya lazima, kuimarisha ujuzi wa vitendo na kuwawezesha wanafunzi kuingia kwenye ajira au kujiajiri.
“Hakuna wizara moja, taasisi, au shule inayoweza kusimamia mahitaji kama haya peke yake. Lazima tupange kwa pamoja, tutarajie kutakuwa na ongezeko la mahitaji ya walimu, madarasa, vifaa vya kujifunzia, fedha na tuhakikishe utekelezaji unalenga mahitaji ya wanafunzi,” amesisitiza.
Kwa upande wake, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda alisema mkutano huo unafanyika katika wakati sahihi ambapo Serikali inasimamia mageuzi katika sekta ya elimu, mageuzi ambayo yana kalenda ya ukalimishaji na tayari safari imeshaanza.
“Mageuzi haya yanalenga kuongeza ujuzi katika elimu ili isiwe ya mafundisho tu ya kinadharia bali impe mwanafunzi uwezo wa kujiajiri. Hapa tuna mkondo wa elimu ya amali na mkondo wa elimu jumla,” alisema.
Akielezea mabadiliko hayo, Prof. Mkenda alisema elimu ya sasa itatoka miaka saba hadi 10 na itakuwa ni ya lazima kwa kila mtoto wa Kitanzania. Watoto lazima wasome hadi kidato cha nne, wazazi lazima wawasimamie watoto. Kwa hiyo, elimu ya msingi itakuwa ya miaka sita, na baada ya hapo inabidi waende kidato cha kwanza,” alisema.
Alisema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alishawapa Wakuu wote wa Mikoa kipimo cha utekelezaji wa agizo lake kuhusiana na maandalizi ya kuanza kwa mfumo huo mpya na kwamba hivi sasa nguvu kubwa inapaswa ielekezwe kwenye suala hilo.
“Kalenda ya utekelezaji imeshatoka na ifikapo Januari, 2028 tutakuwa na wahitimu wa darasa la sita na darasa la saba ambao wote kwa pamoja wataingia kidato cha kwanza. Katika hili hakuna kufeli wala hakuna kurudi nyuma,” alisisitiza.
Alitumia fursa hiyo kuwaalika wadau wa elimu nchini waangalie fursa zilizopo na wapi wanaweza kusaidiana na serikali kufanikisha lengo hilo. “Tunaalika wadau kwa sababu bado tunahitaji shule zaidi. Tunahitaji taasisi za dini na sekta binafsi zituunge mkono.”