Vijana wanaoishi katika maeneo ya mwambao wa Ziwa Victoria wilayani Geita wametakiwa kutumia fursa za kiuchumi zilizopo katika sekta ya uvuvi kwa kuwekeza katika ufugaji wa samaki kwa kutumia vizimba, ili kuongeza kipato na kujikwamua kiuchumi.
Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Wilaya ya Geita, Naomi Fujo, wakati akiendelea na ziara ya kutembelea vikundi vya vijana vilivyonufaika na mikopo ya asilimia nne inayotolewa na halmashauri.

Katika ziara hiyo, amekipongeza kikundi cha vijana cha Kageye kwa kuanzisha mradi wa ufugaji wa samaki kwa kutumia kizimba, chenye samaki zaidi ya 4,000, akisema mradi huo ni mfano wa namna vijana wanavyoweza kutumia fursa zilizopo katika maeneo yao kujiletea maendeleo.
Aidha, amewahimiza vijana hao kuongeza idadi ya vizimba na kutoa elimu kwa vijana wengine kuhusu fursa za ufugaji wa samaki ili kuwahamasisha kuanzisha miradi inayofanana.
Kwa upande wake, Afisa Vijana wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Alex Herman, amesema kikundi hicho chenye wanachama sita, ambao awali walikuwa wakijihusisha na shughuli za uvuvi wa kawaida, kimefanikiwa kupata mkopo wa shilingi milioni 65 kutoka halmashauri hiyo.
Amesema fedha hizo zimewezesha kikundi hicho kuanzisha mradi wa kisasa wa ufugaji wa samaki kwa kutumia vizimba katika Ziwa Victoria, hatua inayotarajiwa kuongeza tija katika shughuli zao za kiuchumi.
Kikundi hicho kinatarajia kupata mapato yatakayofikia mara mbili hadi tatu ya kiasi cha mkopo kilichotolewa na halmashauri, jambo linalotarajiwa kuongeza kipato cha wanachama wake na kuboresha maisha yao kupitia uwekezaji katika sekta ya uvuvi.