Jeshi la Polisi wilayani Sengerema, mkoani Mwanza, limetoa wito kwa wataalamu wa tiba asili na tiba mbadala kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa kufuata sheria, kanuni, na miongozo iliyowekwa na Serikali ili kuongeza ufanisi na kulinda usalama wa jamii.
Wito huo umetolewa na Msimamizi wa Polisi Kata Wilaya ya Sengerema, Mrakibu wa Polisi (SP) Sarakikya Kiongozi, alipokuwa akizungumza na wataalamu hao katika kikao cha uhamasishaji wa mafunzo ya sayansi shirikishi kilichofanyika Novemba 19, 2026, katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema.
Katika hotuba yake, SP Kiongozi aliainisha mambo muhimu yanayopaswa kuzingatiwa na wataalamu hao, ikiwemo kudumisha amani, kufanya kazi kwa kuzingatia misingi ya kisheria ya tiba asili na tiba mbadala, kushiriki mafunzo ya sayansi shirikishi yanayoratibiwa na Chama cha Wataalamu wa Tiba Asili (TAMESOT) kwa kushirikiana na mamlaka za serikali, pamoja na kujenga ushirikiano wa karibu na vyombo vya dola.

Onyo Dhidi ya Vitendo vya Jinai
Sambamba na hayo, afisa huyo wa polisi aliwaonya vikali wataalamu hao kutojihusisha na matukio ya jinai katika utoaji wa huduma zao. Alisisitiza kuwa endapo atatokea mteja anayehitaji tiba zinazohusishwa na matukio ya uhalifu—yakiwemo mauaji au kutaka kinga ili asikamatwe na vyombo vya sheria—wataalamu hao hawana budi kutoa taarifa polisi mara moja.
Alihitimisha kwa kuwahakikishia kuwa Jeshi la Polisi lipo tayari kutoa ushirikiano wa karibu ili kuondoa dhana ya uadui au hofu iliyokuwepo hapo awali kati ya askari na watoa huduma za tiba asili.
Msimamo wa TAMESOT na Wataalamu
Kwa upande wake, Mratibu wa Hamasa na Mafunzo Ngazi ya Taifa ambaye pia ni Katibu Mkuu wa TAMESOT, Bw. Lukasi Joseph Mlipu, akiendesha darasa la uhamasishaji katika kikao hicho, aliwasisitiza wataalamu hao kuzingatia miiko ya kazi yao, kudumisha umoja, upendo, na ushirikiano, huku akiwahimiza kuhudhuria mafunzo rasmi yatakayowawezesha kutoa huduma kwa njia sahihi na salama.

Nao wataalamu wa tiba asili waliohudhuria kikao hicho walipongeza elimu na ujumbe huo kutoka Jeshi la Polisi, wakiahidi kuimarisha ushirikiano, kuachana na hofu isiyo ya lazima dhidi ya askari, na kufanya kazi kwa kufuata miongozo ya kitaalamu.