Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Wilaya ya Geita umewapongeza vijana wanaojishughulisha na shughuli za uzalishaji mali kupitia vikundi vya ujasiriamali, huku ukiwataka vijana wengine kuiga mifano hiyo kwa kutumia fursa za mikopo na taaluma walizonazo kujikwamua kiuchumi.
Akizungumza wakati wa ziara ya viongozi wa UVCCM Wilaya ya Geita iliyolenga kukagua na kujionea shughuli zinazofanywa na vijana walionufaika na mikopo ya asilimia 4Â inayotolewa na Halmashauri, Mwenyekiti wa umoja huo wilayani humo, Naomi Fujo, amekipongeza kikundi cha Meet Point kilichopo Rwezera, Nzera, kwa hatua kilizopiga katika shughuli zake za kiuchumi.

Fujo amesema uamuzi wa vijana kujikita katika shughuli za uzalishaji mali badala ya kutegemea ajira pekee unahitaji moyo, ujasiri na dhamira ya kweli ya kujiletea maendeleo.
Amesema katika ziara hiyo viongozi wa UVCCM walichagua wenyewe vikundi walivyotembelea bila kuelekezwa na viongozi wa maeneo husika, ili kupata taswira halisi ya namna vijana wanavyotumia fursa za uwezeshaji zinazotolewa na Serikali.
Kwa upande wake, Mhasibu wa kikundi cha Meet Point, Fedison Mkufu, amesema mkopo wa Sh milioni 35 walioupata umekuwa chachu ya maendeleo yao kiuchumi kupitia mradi wa ufugaji, ambao umewawezesha kuongeza uzalishaji, kutoa ajira kwa vijana wengine na kuwa mfano wa kujifunza kwa wafugaji wanaoanza.
Naye Afisa Vijana wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Alex Herman, amewahimiza vijana wenye nia ya kuanzisha au kuendeleza miradi ya kiuchumi kufuata taratibu za kuomba mikopo ya asilimia 10, akieleza kuwa ofisi yake iko tayari kutoa elimu na mwongozo kuhusu fursa hizo pamoja na kuwawezesha vijana wengine kunufaika.