Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimekosoa vikali taarifa rasmi iliyotolewa na Serikali ya Tanzania kwenda kwa Serikali ya Uingereza kufuatia hukumu ya miaka minne gerezani iliyotolewa dhidi ya Mwenyekiti wake ngazi ya taifa, Tundu Lissu.
CHADEMA imedai kuwa taarifa hiyo ni ya serikali kujificha nyuma ya kisingizio cha uhuru wa mahakama, mamlaka ya nchi na kutokuingiliwa masuala ya ndani na kwamba taarifa hiyo haiwezi kufuta kile CHADEMA inachodai kuwa ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu na taratibu za kisheria uliojitokeza wakati wa shauri hilo.
Msimamo huo umetolewa Ijumaa, Novemba 13, 2026, kupitia taarifa rasmi kwa umma iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa CHADEMA, Brenda Rupia. Taarifa hiyo ya CHADEMA imekuja kufuatia majibu ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ya Tanzania ya Novemba 12, 2026, iliyozitaka nchi washirika ikiwamo Uingereza kuheshimu uhuru wa mahakama na michakato ya kisheria.
Majibu hayo ya Tanzania yalitolewa baada ya Waziri wa Afrika na Maendeleo ya Kimataifa wa Uingereza, Kirsty McNeill, kutoa tamko mnamo Novemba 10, 2026, akieleza wasiwasi mkubwa wa Uingereza juu ya kutiwa hatiani kwa Lissu katika kesi ya uchochezi kutoka kwenye kesi ya uhaini na kukumbusha maoni ya Kikundi Kazi cha Umoja wa Mataifa kuhusu Uzuiaji Holela wa Uhuru (UN Working Group on Arbitrary Detention, Opinion No. 74/2025).
CHADEMA imeeleza kuwa majibu ya Serikali ya Tanzania yanasikitisha sana na ni taswira ya kiburi cha kidiplomasia kinachokiuka misingi ya demokrasia ya katiba na utawala wa sheria. Chama hicho kimesema kuwa uhuru wa mahakama hautoi kinga dhidi ya ukaguzi halali pale inapobainika kuwa kuna tuhuma nzito za ukiukaji wa taratibu za utoaji haki.
Pia, CHADEMA imekumbusha kuwa Tanzania ni nchi mwanachama wa Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa (ICCPR), ambapo Ibara ya 14 inaratibu na kuhakikisha haki ya mtu kupata fursa ya kusikilizwa kwa haki mbele ya chombo huru na kisicho na upendeleo. Kwa msingi huo, CHADEMA imebainisha kuwa wasiwasi uliotolewa na Uingereza ni mashauriano halali ya kidiplomasia kuhusu wajibu wa kimataifa wa haki za binadamu na wala siyo shambulio dhidi ya mamlaka au uhuru wa mahakama wa Tanzania.
“Majibu ya Serikali yanasikitisha sana. Badala ya kujibu hoja za msingi za kisheria na haki za binadamu zinazohusu kesi, kutiwa hatiani na kuhukumiwa kwa Mheshimiwa Lissu, imekimbilia kutaja uhuru wa mahakama, mamlaka ya nchi na kutokuingiliwa masuala ya ndani”, imeeleza CHADEMA.
CHADEMA imeweka wazi kuwa Serikali ya Tanzania imeshindwa kujibu masuala matano makuu ya kisheria na ya msingi yanayozunguka kesi na hukumu ya Tundu Lissu. Suala la kwanza ni uzuiaji holela wa uhuru ikieleza kuwa Lissu alikamatwa mnamo Aprili 9, 2025, na kuwekwa mahabusu kwa takribani miezi 19 (siku 577) kabla ya kuhukumiwa, hatua inayokiuka misingi ya haki na kupuuza maoni ya Kikundi Kazi cha UN (Opinion No. 74/2025).
Suala la pili ni kunyimwa msaada na uwakilishi wa kisheria ikieleza kuwa haki yake ya kupata fursa ya siri na madhubuti ya kuwasiliana na mawakili wake ilihujumiwa vibaya. Suala la tatu ni kutiwa hatiani kwa kosa mbadala ikieleza kuwa baada ya Mahakama Kuu kumwachia Lissu kwenye kosa la uhaini, ilimtia hatiani kwa kosa la uchochezi chini ya Kifungu cha 390 cha Kanuni ya Adhabu ikitumia Kifungu cha 319 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), bila kumpa notisi na fursa stahiki ya kujitetea dhidi ya kosa hilo mbadala.
Suala la nne ni kunyimwa haki ya kutoa utetezi ikieleza kuwa Lissu hakupewa fursa ya kutosha ya kuleta mashahidi au kujitetea dhidi ya tuhuma zilizotumika kumhukumu, na suala la tano ni kushuka kwa uwazi na kuzuia waangalizi ikieleza kuwa kesi hiyo ilikabiliwa na usumbufu wa kurusha matangazo mubashara pamoja na kuzuia waangalizi wa kujitegemea na wa kimataifa kufuatilia mwenendo wa shauri hilo.
“Swali la msingi linalobaki ni hili: Mtu anawezaje kutiwa hatiani na kuhukumiwa kwa kosa ambalo hakupewa fursa ya kutosha ya kuyapinga madai yake na kutoa utetezi dhidi ya kosa hilo? Hili ndilo swali ambalo mchakato wa rufaa lazima uuchunguze kwa kujitegemea na bila upendeleo,” imeeleza sehemu hiyo ya taarifa hiyo.
CHADEMA imeongeza kuwa wasiwasi juu ya mwenendo wa kesi ya Lissu hauko kwa Uingereza pekee, bali umeripotiwa pia na mashirika mengi ya kimataifa na ya ndani ikiwemo Amnesty International (ambayo ililaani hukumu hiyo mnamo Novemba 6, 2026), International Federation for Human Rights (FIDH), Human Rights Watch, na Kituo cha Haki za Binadamu (LHRC).
Aidha, chama hicho kimesisitiza kuwa kesi hiyo haiwezi kutazamwa kwa kutengwa, bali lazima itazamwe katika muktadha mpana wa matukio ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, yaliyogubikwa na vurugu, tuhuma za mauaji yasiyo ya kisheria, upotevu wa watu kwa nguvu, na madai ya kuminywa kwa uhuru wa kisiasa. Pia kimebainisha kuwa masuala hayo yaliibuliwa wakati wa Tathmini ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa (UPR) mnamo Novemba 5, 2026.
Kutokana na hayo yote, CHADEMA imetoa wito kwa Serikali ya Tanzania na Mamlaka za Nchi kutopuuza kile ilichokiita wasiwasi halali wa kimataifa wa haki za binadamu kama uingiliaji wa mambo ya ndani, mahakama kuhakikisha mchakato wa rufaa unakuwa huru, wa haki na wa wazi unaoheshimu haki za katiba za Lissu, Jumuiya ya kimataifa (ikijumuisha Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika, Umoja wa Ulaya na Jumuiya ya Madola) kuendelea kushikilia msimamo wa kutaka mageuzi ya kidemokrasia na uwajibikaji, mamlaka kuwaachilia wale wanaodaiwa kukamatwa kiholela, kuanzisha uchunguzi huru juu ya ukiukaji wa haki uliotokea katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025, na serikali kuanzisha kile CHADEMA inaita maridhiano ya kweli ya kitaifa na kurejesha mazingira ya siasa za vyama vingi.
“Haki lazima ionekane ikitendeka, siyo tu kutangazwa kwa maneno. Heshima ya Tanzania kimataifa haitaokolewa kwa taarifa za kujitetea, kutoa wito wa mamlaka ya nchi au kutaka kimya cha kidiplomasia, bali itarejeshwa kupitia kuheshimu katiba, uwajibikaji na utoaji haki unaoonekana,” ameeleza Brenda Rupia katika taarifa hiyo.