Mburudishaji na mtengeneza maudhui nchini Tanzania, Nick Reynolds maarufu kama Bongo Zozo ametoa tahadhari dhidi ya kile alichokiashiria kama maridhiano ya juujuu bila kwanza kuelewa na kushughulikia chanzo cha msingi cha mpasuko uliopo katika jamii na siasa za nchi.
Akizungumza katika video aliyoichapisha kupitia ukurasa wake wa mtandao wa Instagram kwa kuzingatia ujumbe na mawazo aliyoyataja kuwasilishwa na Mtanzania aitwaye Suleiman DM, mburudishaji huyo amesisitiza kuwa maridhiano ya kweli hayawezi kupatikana kwa kunywa chai au kupiga picha pekee.
Bongo Zozo amebainisha kuwa kukimbilia maridhiano bila kutambua sababu za mpasuko ni sawa na daktari anayempa mgonjwa dawa bila kwanza kumfanyia uchunguzi au kubaini ugonjwa unaomsumbua.
“Kukimbilia maridhiano bila kuanza kutambua sababu za mpasuko ni hatari kwasababu tunaweza kujikuta tunatafuta umoja bila kutatua matatizo yaliyosababisha kutengana. Maridhiano ya ukweli yanahitaji kwanza kuelewa nini kilitokea, kwanini kilitokea, nani aliathirika na nini kifanyike ili hali hiyo isijirudie”, ameeleza Bongo Zozo.
Ameongeza kuwa jamii haipaswi kuchanganya ukimya na amani, wala kudhani kuwa kutokuwepo kwa malumbano ya wazi kunamaanisha kuwa tayari kuna maridhiano ya dhati
“Tusichanganye ukimya na amani wala tusidhani kwamba kutokuwepo kwa malumbano kunamaanisha kwamba tayari kuna maridhiano… Tusikubali kupeana mikono kinafiki, kunywa chai halafu kila mtu anaondoka zake kana kwamba hakuna kilichotokea zaidi ya picha”, ameeleza.
Akiendelea kusoma ujumbe wa mtu huyo, Bongo Zozo ameeleza sababu tano kuu zinazofanya uelewa wa chanzo cha mpasuko kuwa jambo la lazima kabla ya kutangaza maridhiano. Kwanza ni kutambua chanzo cha tatizo, pili ni kuepuka maridhiano ya juujuu, tau ni kujenga upya uaminifu akieleza kuwa watu waliopoteza imani wanahitaji kusikilizwa na kuona hatua thabiti zikichukuliwa, nne ni kuweka uwajibikaji akieleza kuwa makosa yaliyotokea lazima yatambuliwe na kuwekewa utaratibu wa kuyashughulikia, na tano ni kuzuia migogoro isijirudie akieleza kuwa lazima kuwe na mabadiliko ya kimfumo yanayoshughulikia mizizi ya mgogoro.
Bongo Zozo amebainisha kuwa ingawa mazungumzo ya kutuliza hali yanaweza kuanza mara moja na hayapaswi kucheleweshwa, mazungumzo hayo hayapaswi kuchukua nafasi ya kutafuta ukweli.
Kutokana na hilo, amependekeza hatua tano za kufikia maridhiano ya kudumu. Hatua ya kwanza ni kutambua mpasuko kwa kuelewa historia na mazingira yote yaliyosababisha mgogoro, hatua ya pili ni kusikiliza kwa kutoa fursa na nafasi sawa kwa pande zote kueleza malalamiko na uzoefu wao, hatua ya tatu ni kutafuta ukweli kwa kuchunguza madai na kubaini ukweli kupitia utaratibu huru na unaoaminika, hatua ya nne ni kushughulikia madhara na mifumo kwa kuweka haki, uwajibikaji, kutoa fidia inapostahili na kufanya mageuzi ya kimfumo na hatua ya tano ni kujenga uaminifu kwa kuweka makubaliano rasmi, kuainisha muda wa utekelezaji na kuweka mfumo wa kufuatilia matokeo.
“Maridhiano bila kutambua chanzo cha mpasuko ni kujenga nyumba juu ya msingi usiojulikana… Hatuwezi kutafuta amani ya kudumu kwa kufunika matatizo badala ya kuyatatua. Umoja wa kweli hujengwa kwa ukweli, haki, kusikilizana, uwajibikaji na utayari wa kurekebisha makosa”, ameeleza.
Akitamatisha maelezo yake, Bongo Zozo ameeleza kuwa lengo kuu la maridhiano linapaswa kuwa kujenga Tanzania ambayo wananchi wanaweza kutofautiana kimtazamo na kisiasa bila kuogopana au kuchukiana.
“Tunataka kurudi katika Tanzania ambayo mimi nikivaa jezi yangu ya kijani sina hofu, na akipita kamanda amevaa gwanda lake wala hashtuki. Tuweze kutofautiana kisiasa bila kuogopana. Tuweze kuwa na mawazo tofauti bila kuwa maadui… Inamaanisha kwamba tunaweza kuishi pamoja kwa amani, haki na kuheshimiana licha ya tofauti zetu”, ameeleza Bongo Zozo.