Wizara ya Kilimo imeanza kupitia mapendekezo ya kutungwa kwa Sheria ya Ulinzi na Maendeleo ya Kilimo ya mwaka 2027, hatua inayolenga kuimarisha usimamizi na ulinzi wa rasilimali za kilimo nchini.
Hatua hiyo imefanyika Novemba 20, jijini Dodoma, kupitia kikao kazi cha ushirikiano kati ya Wizara ya Kilimo na wataalamu wa sheria kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria.

Kikao hicho kilichoongozwa na Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa Wizara ya Kilimo, Bi. Angela K. Anatory, kimejadili mapungufu yaliyopo katika mifumo ya sasa ya kisera, kisheria na kitaasisi inayosimamia sekta ya kilimo, pamoja na mapendekezo ya kuweka mifumo madhubuti ya ulinzi wa ardhi ya kilimo, kilimo cha mkataba na zana za kilimo.
Tathmini hiyo inalenga kuweka mazingira bora ya kisheria yatakayochochea ongezeko la uzalishaji, kulinda rasilimali za kilimo na kuhakikisha sekta hiyo inakuwa endelevu na kuchangia zaidi katika ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Maandalizi hayo ni sehemu ya juhudi za kuimarisha mazingira ya kisheria na kitaasisi ya sekta ya kilimo, sambamba na Mwelekeo wa Maendeleo na Mageuzi ya Kilimo chini ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
