Baadhi ya wahudumu wa mabasi (makondakta) waliohitimu mafunzo maalum katika Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) mkoani Mara, wameiomba Serikali kuweka utaratibu utakaowabana wamiliki wa vyombo vya usafiri kutoa kipaumbele cha ajira kwa vijana waliopata mafunzo rasmi ili kujenga heshima, weledi, na nidhamu katika sekta ya usafirishaji.
Wito huo umetolewa katika hafla fupi ya kuwaaga wahitimu 16 wa mafunzo hayo iliyofanyika jana, Novemba 20, 2026, chuoni hapo. Wahitimu hao walikiri kuwa kwa muda mrefu wamekuwa wakitekeleza majukumu yao kwa mazoea bila kuwa na taaluma rasmi, hali iliyokuwa ikisababisha migogoro ya mara kwa mara baina yao na abiria kutokana na baadhi yao kutotumia lugha zenye staha.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Chuo cha VETA Mara, Bw. Martin Maollel, aliunga mkono hoja hiyo na kuwataka wahitimu hao kwenda kuwa mabalozi wazuri kwa kutoa huduma bora na za kisasa kwa abiria.
Aidha, Bw. Maollel aliwasisitiza kuzingatia mawasiliano mazuri na yenye ushirikiano kati yao na madereva wao wakati wote wa safari, sambamba na kuhakikisha usalama na usimamizi madhubuti wa mizigo ya abiria.
Kwa upande wake, Afisa Mfawidhi wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) Mkoa wa Mara, Bw. George Robert, alieleza kuwa mamlaka hiyo imekuja na mkakati maalum wa kutoa elimu kwa makondakta ili kuwajengea heshima na hadhi inayofanana na watoa huduma wengine katika mashirika makubwa ya usafirishaji.
Nao baadhi ya wanufaika wa mafunzo hayo waliipongeza Serikali kupitia VETA na LATRA kwa kuanzisha programu hiyo, wakieleza kuwa imewafungua macho na kuwapa mbinu mpya za kuhudumia wateja kwa weledi.