Wananchi mkoani Iringa wamelipongeza Jeshi la Polisi mkoani humo chini ya uongozi wa Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Allan Bukumbi, kwa juhudi zake za kuimarisha ulinzi na usalama pamoja na kuwashirikisha wananchi katika shughuli mbalimbali za kuboresha huduma za kipolisi.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi, Joseph Mgongolwa amesema kuwa katika kipindi cha uongozi wa Kamanda Bukumbi, jeshi hilo limefanikiwa kurejesha imani na heshima kwa wananchi, tofauti na ilivyokuwa awali ambapo baadhi ya wananchi walikuwa wakilitazama jeshi la polisi kama adui badala ya mshirika wao katika masuala ya usalama.

Aidha Mgongolwa amempongeza Kamanda Bukumbi kwa kuwafikia wananchi kupitia kampeni ya “Ongea na Kamanda” inayotekelezwa kata kwa kata, akisema mpango huo umekuwa fursa muhimu ya kusikiliza maoni, malalamiko na kero za wananchi ili kuzitafutia ufumbuzi na kuboresha mahusiano kati ya polisi na jamii.
Mbali zaidi amepongeza juhudi za uongozi huo katika kushirikisha wadau mbalimbali wa maendeleo wanaochangia kuboresha miundombinu na vitendea kazi vya jeshi hilo, ikiwemo ujenzi wa vituo vipya vya polisi, ukarabati wa vituo vya zamani pamoja na upatikanaji wa magari kwa ajili ya kurahisisha utekelezaji wa majukumu ya kiusalama.

Amesema ushirikiano huo ni muhimu katika kuhakikisha jeshi la polisi linakuwa na mazingira bora ya kufanyia kazi na kuongeza ufanisi katika kuwahudumia wananchi, huku akiwahimiza wakazi wengine wa Iringa kuendelea kuunga mkono juhudi zinazofanywa na jeshi hilo katika kulinda amani na usalama wa mkoa.
Kwa upande wake, mwananchi mwingine, Maximillian Lugenge, mbali na kupongeza utendaji wa Kamanda Bukumbi, ametoa ombi kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) Camillus Wambura kumwongezea muda wa kulitumikia jeshi hilo iwapo taratibu na mazingira yataruhusu.
Lugenge amesema hatua hiyo itakuwa na manufaa kwa jeshi la polisi na jamii kwa ujumla, kutokana na mchango ambao Kamanda Bukumbi ameendelea kuutoa katika kuimarisha uhusiano kati ya polisi na wananchi pamoja na kuboresha masuala ya ulinzi na usalama.
Kwa ujumla, wananchi hao wameeleza kuwa ushirikiano, usikivu na uwajibikaji wa jeshi la polisi ni msingi muhimu wa kujenga imani kwa jamii, huku wakihimiza juhudi hizo kuendelezwa ili kuhakikisha mkoa wa Iringa unaendelea kuwa salama na wenye amani.