Miili 36 iliyochukuliwa vinasaba katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC) kutokana na ajali ya basi la Kampuni ya Channel One na Coaster kugongana na kuwaka moto Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro inakabidhiwa kwa ndugu wa marehemu huku miili mingine miwili zoezi la kuchukua vinasaba linaendelea na miili hiyo itakabidhiwa kwa ndugu baada ya zoezi kukamilika.
Wanafamilia, marafiki na wananchi wanashiriki katika tukio hilo katika viwanja vya KCMC kwa ajili ya kukabidhiwa miili ya ndugu zao. Majeneza yenye miili ya watu 36 kati ya 42 yamewekwa sehemu maalum ambapo wataagwa kimkoa na kisha kukabidhiwa familia kwa taratibu za maziko.
Ajali hiyo ilitokea Juni 28, 2025 katika eneo la Sabasaba, Same mjini ikihusisha basi kampuni ya Chanel One lililokuwa likitokea Moshi kwenda Tanga na basi dogo aina ya Coaster lililokuwa likitokea Same Mjini kwenda Moshi kugongana uso kwa uso na kuwaka moto wakati abiria wakiwa ndani ya magari hayo.
Katika mfululizo wa taarifa za ajali hiyo zilizokuwa zikitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu zilieleza kuwa waliofariki kwenye Coaster ni watu 31 ambao kati yao wanawake ni 21 na wanaume ni 10, huku kwenye basi la Chanel one wakifariki watu 11 na hivyo kufanya jumla ya waliofariki kufikia 42.