Latest Posts

ASKOFU MWAMAKULA ATUMA WARAKA WA WAZI KWA RAIS SAMIA, AGUSIA KATIBA

Askofu Mkuu wa Kanisa la Moravian la Uamsho Tanzania Askofu Emmaus Bandekile Mwamakula leo, Jumamosi Novemba 09.2024 ametupa waraka wa wazi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhusiana na sintofahamu inayoendelea kwenye mchakato wa uchaguzi wa serikali za mitaa 2024

Kupitia waraka huo, Askofu Mwamakula ametoa wito kwa Rais Dkt. Samia kuingilia kati na kutafuta mwarobaini wa masuala yanayoendelea nchini yatokanayo na uchaguzi huo ambapo amedai kuwa zaidi ya asilimia 95 ya wagombea wa vyama vya upinzani nchini wameenguliwa, na hili ndilo andiko lenyewe sasa:-

“Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan!, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania!, Amani iwe kwako!, pokea salaam za heri kutoka kwetu sisi tulio Askofu tusimamao mbele yako katika zamani hizi kwa ajili ya kuisema dhamira ya dhamiri ambayo dhamira yake haihojiwi na haipingwi na binadamu yeyote”

 

“Mheshimiwa Rais, leo tunakuandikia kuhusu mambo ambayo yako wazi Kikatiba, lakini kwa kuwa baadhi ya watu walioapa mbele ya Rais ili kuilinda Katiba na wengine ambao wametakiwa kusimamia, kutenda na kuyatimiza majukumu yao kwa mujibu wa Katiba; wameamua kwa makusudi kuidharau Katiba; hivyo kusimamia, kutenda na kutimiza majukumu yao kwa utashi na maelekezo yaliyo kinyume na katiba yetu”

“Kwa sababu hiyo Mheshimiwa, taasisi ya Urais ndiyo pekee iliyobaki ambayo Askofu tunaweza kusemezana nayo kwani tunaamini kuwa inayo hofu ya Mungu juu ya wakfu wa Katiba hasa ni kwa sababu Mungu aliitumia Katiba hiyo ili Rais aliyepo akalie kiti cha Urais”

“Mheshimiwa Rais, tunataka usikie malalamiko, masikitiko, kilio, chuki na huzuni kutoka kwa wananchi na wapiga kura juu ya kile ambacho Wizara ya TAMISEMI ilifanya 8 Novemba 2024, ama TAMISEMI ilielekeza kuengua wagombea wote wa upinzani walioomba kuwania nafasi mbalimbali katika uchaguzi huu wa serikali za mitaa 2024 au TAMISEMI imetekwa nyara na kikundi cha watu kinachofanya uhuni huo wa kuengua wagombea kwa sababu na maslahi ambayo hayako wazi”

“Kwamba wameenguliwa zaidi ya 95% ni jambo la kushangaza sana na hao walioachwa ni kwa sababu mazingira ya mitaa hiyo hayakuruhusu waenguliwe (waliogopa kufanyiwa fujo) lakini pia kuna watu wachache walikaidi maelekezo, wengine walioachwa ni wale ambao waliona ni ama wasingeshinda ama waliachwa wajumbe ambao wasingekuwa na nguvu katika serikali ya mtaa yenye Mwenyekiti kutoka CCM nk”

“Mheshimiwa Rais, yaliyotokea jana yanaweza kutafsiriwa kwa namna mbili na sio vinginevyo, ama hayo yalifanyika kwa maelekezo maalum kutoka kwa Rais mwenyewe au TAMISEMI ndio imedhamiria kumhujumu na kumchafua Rais”

“Mheshimiwa Rais, yaliyotendeka hayawezi hata kidogo kumpa sifa Rais ndani na nje ya nchi na ziada ni kuwa wananchi watazidi pia kuichukia serikali inayoongozwa na CCM ambapo wewe ndiye Mwenyekiti wake na Rais wa Tanzania”

“Miezi michache kabla Mzee Kinana hajajiuzulu nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara) tulikutana katika mkutano mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo na tulipata fursa ya kuteta juu ya sheria za uchaguzi na miswada iliyokuwa ikibishaniwa, Mhe. Kinana alitueleza sana juu ya adhma na dhamira ya Rais kuwa uchaguzi wa serikali za mitaa 2024 na uchaguzi mkuu wa 2025 utakuwa huru na wa haki, hii ilitutia moyo sisi ambao kila wakati tunafanya kazi ya kuwatuliza wapinzani wanaohisi kuumizwa”

“Mheshimiwa Rais, katika nchi yeyote ambayo upinzani ukihujumiwa lakini hauchukui hatua za ziada zenye kutumia nguvu kudai haki zao sio kwa sababu hawawezi; bali ni kwa sababu Mungu anaweza kuinua watu wa kuwatuliza na kushauriana nao juu ya njia za kudai haki kwa amani na kwa misingi ya Katiba yao, lakini sio mara zote watu wa aina hiyo watakuwepo au pia watasikilizwa, na ikifikia hatua washauri na hasa wanaoshauri upinzani kutotumia nguvu wakiachwa kusikilizwa inakuwa shida kubwa”

“Tulipokutana (Askofu Bagonza, Fr. Kitima na Askofu Mwamakula) na Waziri Mkuu Kasim Majaliwa majira kama haya mwaka jana jijini Dodoma alitueleza juu ya dhamira njema ya Rais na tulishiba na kuondoka na matumaini, sisi wengine tulijitahidi kusaidia dhamira hiyo njema ili idhihirike kimatendo zaidi kusudi Taifa letu litoke katika mkwamo wa kisiasa wa miaka ipatayo 9 sasa”

“Kama hayo hayatoshi, 4R’s za Rais Samia nazo pia zilileta hamasa na matumaini mapya hivyo kuifunua zaidi nadharia ya dhamira hiyo njema ingawa sisi wengine tuliwahi kuhoji kama hao wateule wa Rais walizielewa hizo 4R’s kwani wengi walitenda kinyume na walichokisema”

“Mheshimiwa Rais, makusudi ya kuuhujumu mchakato wa uchaguzi huu yalianza kujitokeza tangu mwanzo kwani hakukuwepo uwazi katika kuanzisha mchakato, ubaguzi katika kuwateua watoa elimu ya mpiga kura na pia kulikuwa na ‘uhuni’ wa wazi katika zoezi la uandikishaji kwa sababu kulikuwepo malalamiko ya kuandikisha marehemu, watoto na hata watu wasiojulikana maeneo husika, viongozi wa upinzani ambao walihoji ‘uhuni’, walikamatwa na Jeshi la Polisi”

“Mheshimiwa Rais, Waziri wa TAMISEMI jana amesema wasioridhika na uteuzi wakate rufaa lakini inajulikana kuwa pamoja na malalamiko mengi wakati wa zoezi la uandikishwaji kuwa wazi katika mitandao ya kijamii Waziri mwenye dhamana hakuwahi hata siku moja kukemea hujuma na hata yeye mwenyewe au wasaidizi wake hawakuwahi kutoa maelekezo ya wazi ya kurekebisha”

“Ilitarajiwa kabla ya kutoa kauli ya watu kukata rufaa ilibidi Waziri wa TAMISEMI atoe kauli ya kukemea uhuni uliofanywa na watu wake huku chini lakini hii ni aibu kubwa kwa wasimamizi wasaidizi kudharau mchakato huu wa Kikatiba”

“Baada ya kusema hayo Mheshimiwa Rais, sisi Askofu Mwamakula tunajisikia msukumo wa kusema kuwa dalili za kuitumbukiza nchi yetu katika machafuko zimeanza kutoa harufu na sasa mtu anaweza pia kuzigusa kwa mikono”

“Kwamba kuna watu wamejawa kiburi cha kuwa na madaraka na hivyo hawajali jambo lolote na kuwa wako juu ya mtu yeyote na hawawezi pia kuchukua ushauri wa mtu yeyote na pia hakuna mtu yeyote atakayewakemea, inaonekana watu hawajaona funzo kutoka kwa timu ambayo pia ilijinasibu haifungiki lakini ilikuja kudhalilishwa!”

“Mheshimiwa Rais, nchi ikifikia mahali ambapo wateule wa Rais hawajali kelele za wapiga kura kwa sababu ya kutegemea nguvu ya vyombo vya dola inakuwa imeuanza mwanzo wa safari ya mwisho kama haijafikia katikati ya mwanzo wa safari ya mwisho, lakini uzoefu huonyesha kuwa hakuwi na mwisho mwema kwa viongozi na watawala ingawa wananchi huumia zaidi”

“Sisi Askofu tunaona wajibu wetu kumtia moyo Rais ili akumbuke alikotoka anapotazama kule anakoelekea kusudi aweze kulivusha Taifa hili kwa heshima na utukufu mwingi, kinyume cha hayo ni aibu, fedheha, kilio, majonzi na hata pia mahangaiko yanayotukaribia sisi sote”

“Je, nini kifanyike ili heshima na uadilifu katika uchaguzi wa serikali za mitaa 2024 virudi tena, hii ndiyo kazi ya washauri wa Rais, waaminifu na wakweli kufanya, kwa TAMISEMI kurejesha wote walioenguliwa kutasaidia lakini kuondoa pia maelekezo ya kutaka kuibeba CCM katika uchaguzi itakuwa ni tiba zaidi”

“Katika jamii na nchi zinazojali maoni ya wapiga kura na wananchi wake, tusingehitaji shinikizo la Askofu kwani kwa mambo yaliyotokea, Waziri mwenye dhamana angeshajiuzulu kwa ajili ya kulinda heshima ya serikali yake, tunayasema haya Mheshimiwa Rais sio kwa sababu ya wivu au chuki kwa mtu, watu au kikundi cha watu la hasha, sisi tunayasema haya kwani tunaamini kuwa tusiposema, wengi wataogopa kusema, ole wetu sisi tukinyamaza na kumficha Rais!”

“Ni matumaini yetu kuwa waraka huu utafikia katika masikio ya washauri wa Rais walio na unyenyekevu wa kuiona hofu na tahadhari ya Askofu Mwamakula, ni matarajio yetu zaidi pia kuwa Mheshimiwa Rais atapata fursa ya yeye mwenyewe kusoma na kutafakari maudhui ya waraka utokao kwetu sisi Askofu tulio wadogo sana miongoni mwa maaskofu wadogo”;

Na huo ndio mwisho wa waraka husika.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!