Kuelekea Uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 27,2024 Mkuu wa Wilaya ya Tandahimba Kanali Michael Mntenjele amewasisitiza wananchi kuendelea kudumisha amani iliyopo kwenye eneo hilo.
Mntenjele ametoa msisitizo huo kwenye kikao cha kutoa maelekezo ya uchaguzi yaliyotolewa na Msimamizi wa uchaguzi wa Halmashauri hiyo DCI. Mariamu Mwanzalima kilichofanyika kwenye ukumbi wa halmashauri hiyo.
Amesema katika kipindi chote cha uchaguzi ni muhimu kuzingatia amani na utulivu na kuepuka kutumia kigezo cha uchaguzi kwaajili ya kuhatarisha amani iliyopo.
“Hatutakuwa tayari kuona mtu yoyote anahatarisha usalama na amani katika eneo letu,lengo tufanye uchaguzi uliona amani na utulivu kila mtu aweze kutekeleza wajibu wake na haki yake ya kidemoklasia mpaka hapo tutakapopata viongozi baada ya tarehe 27,2024.”Amesema Mntenjele
Kwa upande wa viongozi wa vyama pinzani kwenye halmashauri hiyo ikiwemo Katibu Mwenezi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA Hamisi Bakari ameomba uchaguzi huo uwe wa uwazi na haki ili amani iendelee kuwepo kwani huwezi kudai amani bila kutenda haki.
Naye msimamizi wa uchaguzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tandahimba DCI.Mariamu Mwanzalima amewahimiza kuchukua fomu ya kugombea wakazi wote wanaotaka kugombea nafasi mbalimbali za uongozi wenye umri kuanzia miaka 21 au zaidi ikiwemo nafasi ya Mwenyekiti wa kijiji,wajumbe wa halmashauri ya kijiji na mwenyekiti wa kitongoji.
Ameongeza kuwa kuanzia Novemba 1 hadi 7,2024 ni tarehe ya kuchukua na kurudisha fomu kwa watia nia ya kugombea ambapo uteuzi wa wagombea utafanyika Novemba 8,2024 siku moja baada ya kukamilika kwa zoezi la kurudisha fomu.
Hata hivyo kwa mujibu wa kanuni zoezi la uandikishaji kwenye daftari la kudumu la mpiga kura litafanyika Oktoba 11hadi 20,2024 katika vituo vilivyopangwa huku wakazi wenye sifa za kupiga kura ni kuanzia miaka 18 au zaidi na uchaguzi huo unatarajia kufanyika Novemba 27,2024.