Diwani wa kata ya Mayanga Arif Suleiman Premji ameitaka jamii kuweka jitihada na kuendelea kuhamasika kuwekeza kwenye elimu ili watoto waweze kupata elimu itakayowasaidia katika maisha yao.
Akizungumza wakati wa kusoma Taarifa ya Utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi CCMÂ kwa mwaka 2020-2025 Kata ya Mayanga iliyopo Halmashauri ya wilaya ya Mtwara mkoani Mtwara.
Arif amesema miongoni mwa changamoto zilizopo katika kata hiyo ni baadhi ya wanajamii kuwa na ushirikiano duni kwenye kuwekeza katika elimu hivyo ameiomba jamii kuhakikisha wanaweka jitihada za kuwekeza katika elimu.
Arif ameongeza kuwa katika kipindi cha miaka mitano amechangia zaidi ya shilingi milioni 279 kufanikisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo ndani ya kata hiyo.
Hata hivyo katika kipindi cha uongozi wake Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wameweza kuchangia shilingi bilioni 7 ili kuchochea miradi mbalimbali ya maendeleo katika jamii.
Fedha hizo zimetumika kwa ufanisi katika sekta muhimu ikiwemo sekta ya elimu kwa kutekeleza ujenzi wa madarasa, bweni na vyoo kwa gharama ya shilingi bilioni 1.8 pia ujenzi wa miundombinu ya barabara, maji na umeme kwa zaidi ya shilingi bilioni 5 na upande wa afya imefanikiwa kuboresha vituo vya afya na vifaa kwa gharama ya zaidi ya shilingi milioni 460.
Sambamba na hayo Arif alitumia kikao hicho kuwaaga wananchi wa kata ya Mayanga kwa kutogombea tena nafasi ya Udiwani na badala yake ifikapo Juni 28,2025 atachukua fomu ya kugombea nafasi ya juu zaidi ili azidi kuwatumikia wananchi kwa ukubwa zaidi.
Nao baadhi ya wajumbe na wananchi wa kata hiyo wameonyesha kufurahishwa na utendaji kazi bora wa diwani huyo na wamemtakia kila la kheri kwenye hatua nyingine ya juu anayo ipiga na kuahidi kumuunga mkono na kumtaka diwani atakae pita afanye kazi kama huyu anaetoka.