Latest Posts

AIRTEL MONEY, BUNI NA DTBI WAWAWEZESHA VIJANA KUPITIA MAFUNZO YA IOT

Dar es Salaam: Airtel Money kwa kushirikiana na Buni, Dar Teknohama Business Incubator (DTBI), Vocalize IoT Project na Techstar Innovation Hub, wameendesha mafunzo ya Internet of Things (IoT) na Digital Literacy kwa wanafunzi kutoka vyuo vikuu na VETA nchini.

Mafunzo hayo yamelenga kuwajengea vijana uwezo wa kutumia teknolojia na ubunifu kutengeneza suluhisho za kidijitali zinazoweza kutatua changamoto za jamii, kuongeza fursa za kujiajiri na kuchochea ajira kupitia uchumi wa kidijitali.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Meneja wa Huduma za Kifedha, Miamala ya Kigeni na Majukwaa ya Kidijitali wa Airtel Money, Rita Nyamwehura, amesema kampuni hiyo inaendelea kuwawezesha Watanzania kutumia huduma za kifedha za kidijitali kwa usalama na urahisi.

Nyamwehura amesema vijana wanapaswa kutumia fursa zinazotokana na teknolojia, ikiwemo huduma za Airtel Money kama vile kununua vifurushi, kulipa bili na kufanya malipo kupitia Lipa Namba.

“Tunaamini teknolojia za kidijitali ni chachu ya ukuaji wa uchumi na fursa kwa vijana. Kupitia ushirikiano huu, tunataka kuwawezesha vijana kutumia ubunifu wao kutengeneza suluhisho zinazogusa maisha ya kila siku ya Watanzania,” amesema Nyamwehura.

Kwa upande wake, Business Development Manager wa JATEC, Elia Kinshaga, amesema mafunzo hayo yanalenga kuwajengea vijana uwezo wa kubuni teknolojia za IoT zinazoweza kutumika katika sekta mbalimbali, zikiwemo afya, usalama, usafirishaji na usimamizi wa maji.

Kinshaga ametolea mfano matumizi ya mita janja za maji zinazolipiwa kabla ya matumizi, akisema teknolojia hiyo inaweza kusaidia kupunguza upotevu wa mapato, kuongeza uwazi na kuboresha utoaji wa huduma.

Amesema kupitia ushirikiano wa Airtel na DTBI, zimeanzishwa Fursa Labs, zikiwa na vifaa vya TEHAMA, intaneti na maabara za ubunifu zinazowawezesha vijana kubuni, kujaribu na kukuza bidhaa za kiteknolojia.

Ameongeza kuwa miongoni mwa mafanikio ya maabara hizo ni mfumo wa Visomo, unaomilikiwa na MagilaTech, ambao umewezesha wanafunzi wa VETA kupata elimu kwa njia ya mtandao na sasa unatumika Tanzania pamoja na masoko ya kimataifa, ikiwemo Dubai na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Kwa upande wao, baadhi ya washiriki wamesema mafunzo hayo yamewasaidia kuelewa namna teknolojia ya IoT inavyoweza kutumika kutatua changamoto za jamii na kuanzisha biashara za kidijitali.

Mmoja wa washiriki, Levina Chifiye, mwanafunzi wa St. Joseph College of Engineering and Technology, amesema amepata uelewa kuhusu matumizi ya IoT katika sekta za usalama, usafirishaji na mifumo ya malipo.

Amesema pia huduma za Airtel Money API zinaweza kuwasaidia wabunifu kuunganisha mifumo ya malipo katika miradi yao ya kiteknolojia.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!