Latest Posts

DKT. MPANGO: TEHAMA SULUHISHO LA KUKOMESHA UBADHIRIFU KATIKA UNUNUZI WA UMMA

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Phillip Mpango, ameagiza Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) kuhakikisha kuwa ununuzi wa umma unafanyika kupitia mfumo wa kielektroniki- NeST, ili kudhibiti ubadhirifu na upotevu wa fedha za umma.

Dkt. Mpango alitoa agizo hilo alipotembelea banda la PPRA kabla ya kufungua Mkutano wa Tano wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) unaofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC), Februari 11 – 13, 2025.

Akizungumza baada ya kusikiliza maelezo ya Mkurugenzi Mkuu wa PPRA, Bw. Dennis Simba, kuhusu ufanisi wa Mfumo wa NeST ulioanza kutumika Julai 1, 2023, Makamu wa Rais alisema mifumo thabiti ya TEHAMA inaweza kuwa suluhisho la kuzuia ubadhirifu unaofanywa na baadhi ya watu, aliowafananisha na “mchwa”.

“Fedha nyingi za umma – karibu asilimia 80 – hutumika kwenye ununuzi. Kwa hiyo, nategemea PPRA mtusaidie kupunguza au kuondokana kabisa na matatizo haya. Naamini mifumo ya kimtandao itatusaidia kukomesha wachwa wanaoharibu ununuzi wa umma,” alisema Dkt. Mpango.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa PPRA, Bw. Dennis Simba, alisema mamlaka hiyo imeanza kutekeleza maagizo ya Makamu wa Rais kwa kuweka vizuizi vya ki-TEHAMA kwenye Mfumo wa NeST ili kuzuia udanganyifu na ubadhirifu unaojitokeza kwenye Ripoti za Ukaguzi.

“Mfumo wa NeST sasa umeimarishwa na mageti ya kudhibiti mianya ya ufisadi. Kwa mfano, mkataba hauwezi kutoka bila kusainiwa na Bodi ya Zabuni, na ripoti ya Kamati ya Tathmini lazima isainiwe na wajumbe husika,” alieleza Bw. Simba.

Hadi sasa, mikataba yenye thamani ya Shilingi Trilioni 14 imekwishatolewa kupitia Mfumo wa NeST tangu ulipoanzishwa, huku changamoto kubwa ikiwa ni uelewa wa mfumo huo kwa watumiaji wake.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!