Latest Posts

DP WORLD YATOA UFAFANUZI KUHUSU TUHUMA ZA HUDUMA HAFIFU

Kumekuwa na taarifa zinazozagaa mitandaoni zikidai kuwa huduma zinazotolewa na kampuni ya DP World Dar Es Salaam kwa kampuni za meli za Emirates Shipping Line na MSC – Mediterranean Shipping Company ni za kiwango cha chini. Katika kufafanua suala hilo, mamlaka husika zimeeleza kuwa taarifa hizo si sahihi.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Ofisi ya Mawasiliano na Uhusiano ya DP World, bandari ya Dar Es Salaam ina jumla ya magati 11. Magati namba 0 hadi 7 yanayoendeshwa na DP World yanahudumia meli za magari, mzigo wa kichele, mzigo mchanganyiko na makasha, huku magati namba 8 hadi 11 yakiendeshwa na mtoa huduma mwingine na kuhudumia meli za makasha pekee.

Katika maelezo yao, DP World imethibitisha kuwa kampuni ya Emirates Shipping Line haitumii huduma zao, na kwamba kampuni ya MSC ndiyo inayotumia huduma zao. Kati ya Mei 2024 na Januari 2025, DP World ilihudumia meli 97 za makasha na kushusha na kupakia zaidi ya makasha 217,000. Kiasi hiki kilichangia bandari ya Dar Es Salaam kuvunja rekodi kwa kuhudumia makasha zaidi ya milioni moja kwa mwaka 2024, ikiwa ni ongezeko la asilimia 5 ikilinganishwa na mwaka 2023.

Taarifa hiyo inaeleza zaidi kuwa kabla ya kuanza kwa shughuli za DP World, bandari ya Dar Es Salaam ilikuwa ikipokea meli 3 hadi 4 za MSC kwa mwezi. Hata hivyo, baada ya maboresho ya ufanisi, meli hizo sasa zimeongezeka na kufikia meli 8 kwa mwezi. Kwa mujibu wa DP World, maboresho haya yamechangia meli kuingia bandarini bila kusubiri kwa zaidi ya siku mbili, na kwa baadhi ya meli, kuingia moja kwa moja.

Mabadiliko hayo yamechochea uamuzi wa MSC kuondoa tozo ya ucheleweshwaji wa meli (vessel delay surcharge) mwishoni mwa mwezi Desemba 2024, hatua iliyowapunguzia waagizaji gharama ya takribani dola 500 za Kimarekani kwa kila kasha.

Kuhusu meli ya MSC Imma, iliyotajwa kwenye taarifa za mitandao ya kijamii, DP World imesema meli hiyo ilikuwa na makasha 150 tu kwa ajili ya Dar Es Salaam na haikupangwa kuingia bandarini kwa maombi ya kampuni ya MSC.

Wakati huo huo, wadau wa sekta ya uchukuzi wameendelea kuonesha ushirikiano unaoonekana kwenye ongezeko la mzigo kwa asilimia 12. DP World imewataka wadau na wananchi kwa ujumla kutafuta taarifa sahihi kutoka vyanzo vya kuaminika ili kuepuka usambazaji wa taarifa potofu ambazo zinaweza kudhoofisha jitihada za kukuza sekta ya uchukuzi na uchumi wa taifa kwa ujumla.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!