Serikali, kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT), inatarajia kuanza kutoa elimu ya fedha kwa watoto wadogo ili kuwafundisha umuhimu wa kuweka akiba na matumizi sahihi ya fedha.
Lengo kuu ni kuhakikisha watoto wanajifunza thamani ya fedha na kufanya maamuzi sahihi ya kifedha, ikiwa ni pamoja na matumizi bora ya mikopo wanayoweza kupewa baadaye.
Hayo yamesemwa na Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi (NEEC), Beng’i Issa, alipokuwa akifungua mafunzo ya wiki moja ya uongozi na usimamizi jumuishi kwa wanawake yanayofanyika katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere, Kwamfipa Kibaha.
Beng’i alisema kuwa elimu ya fedha ni muhimu sana, hasa kwa watoto wadogo, ili waweze kujifunza kuweka akiba na kutumia fedha kwa umakini. Alisisitiza kuwa watoto wakifundishwa tangu wakiwa wadogo, itakuwa vigumu kwao kubadilisha tabia hizo wanapokuwa wakubwa.
“Elimu ya fedha katika jamii yetu bado ipo chini sana, hivyo ni muhimu wanawake, ambao ni walezi wakuu wa familia, waanze kutoa elimu ya fedha kwa watoto wao wakiwa bado wadogo,” alisema Beng’i.
Aidha, alisema kuwa ni muhimu elimu ya fedha ianzie shuleni ili kuwaandaa vijana kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi. Aliongeza kuwa kupitia juhudi za Benki Kuu, serikali inafanya mipango ya makusudi kuhakikisha elimu ya fedha inatolewa kuanzia shule za msingi.
“Elimu ya fedha ni muhimu na sasa itaanza kufundishwa kwa mpango maalum kupitia Benki Kuu, kuanzia ngazi za shule za msingi,” alisema Beng’i.
Pia aliwataka wazazi kushiriki kikamilifu katika kufundisha watoto wao umuhimu wa kuweka akiba, akisema kuwa malezi ya kifedha ni muhimu katika kuhakikisha watoto wanakuwa na ufahamu wa fedha tangu wakiwa wadogo.
Kwa upande mwingine, Beng’i alibainisha kuwa serikali inaendelea kuboresha miundombinu muhimu kama vile umeme, maji, na barabara, ili kuwawezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji na kukuza uchumi wa taifa.
Aidha, aliwahimiza wananchi kuchagua viongozi bora katika uchaguzi ujao wa Serikali za Mitaa, huku akiwataka wanawake kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi za uongozi ili kuonyesha umahiri wao katika kutumikia jamii.
Kanali Mstaafu Joseph Simbakalia, aliyeshiriki katika mafunzo hayo, alisema kuwa wanawake ni wawezeshaji wakubwa katika jamii kutokana na malezi wanayotoa tangu wakiwa wadogo. Alisema mafunzo hayo yatawafanya wanawake kuwa imara zaidi katika uongozi.
Kwa upande wake, Meneja wa Idara ya Mafunzo na Ustawi kutoka Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere, Kabula Igambwa, alisema kuwa mafunzo hayo yatasaidia kuboresha uongozi shirikishi kwa wanawake na kuwajengea ushindani katika nafasi za uongozi.