Mwanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Wilaya ya Same Andrew Mchome amelaani kauli ya Makamu Mwenyekiti wa chama hicho John Heche kutangaza kwamba ataandikia barua FIFA ili wasitishe mashindano ya AFCON nchini Tanzania kwa madai ya kuwepo kwa vikundi vilivyopanga kufanya vitendo vya kigaidi.
Hatua hiyo imekuja kufuatia Jeshi la Polisi nchini Tanzania kuwakamata watuhumiwa kadhaa katika maeneo mbalimbali ya nchi wanaodaiwa kujihusisha na vitendo vya kigaidi licha ya kwamba bado vitendo vyao havijathibitishwa Mahakamani
Akizungumza na waandishi wa Habari Leo Julai 29, 2026 Jijini Dar es Salaam Mchome amesema kauli ya Heche ni ya kupingwa kwa sababu inachafua taswira ya nchi kimataifa, na kuongeza kuwa hakuna chama chochote cha siasa kinachopinga maendeleo ndani ya nchi yake hivyo kitendo cha Heche kujitokeza hadharani na kudai ataiandikia FIFA barua kupinga kufanyika kwa AFCON si cha kiungwana
“Juzi nimemsikia akizungumza anasema kwamba tutaandika barua FiFa kuzuia mashindano ya AFCON kutokana na kuwepo kwa viashiria vya UGAIDI, kilichopo kwenye nchi yetu sasa hivi ni kwamba, Kuna watu ambao wana tuhuma ya kupanga vitendo hivyo lakini hakuna Mahakama iliyohukumu mtu kutokana na vitendo vya UGAIDI” amesema mchome
Ameongeza kuwa Kauli ya Makamu mwenyekiti huyo sio ya kizalendo kwa taifa na yaweza kutia hofu wageni wanaotamani kuja kuwekeza nchini lakini pia kutembelea vivutio vya utalii.
Mchome amemtaka Heche kuacha kukigombanisha chama chao na wananchi kwani anaamini kupitia mashindano hayo ya AFCON watanzania wataenda kunufaika kwa namna moja ama nyingine kupitia ugeni mkubwa utakao kuwa nchini.
“Mpenda maendeleo yeyote hawezi kuwa na roho kama hiyo ya kupinga Maendeleo, ugeni utakaoingia nchini utasaidia hadi mamalishe kupata ridhiki zao, pia utafungua ukurasa mwingine kwenye sekta ya utalii” amesema mchome