Katika maadhimisho ya Siku ya Demokrasia Duniani yaliyofanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kuandaliwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) siku ya Jumamosi Septemba 14, 2024, viongozi wa kitaifa na kimataifa wametoa maoni kuhusu changamoto zinazokumba mfumo wa uchaguzi wa Tanzania na jinsi ya kuboresha hali hiyo.
Katika hotuba zao, walielezea matatizo yanayotokana na mfumo wa kisheria, kiutendaji, na kifedha, huku wakipendekeza hatua za kuboresha hali ya demokrasia nchini.
Catherine Ruge, Katibu Mkuu Taifa wa Baraza la Wanawake Chadema (BAWACHA), alizungumzia changamoto kubwa zinazowakabili wanawake, vijana, na watu wenye ulemavu katika uchaguzi.
“Changamoto kubwa ni mfumo wetu wa uchaguzi sheria zetu za uchaguzi hazimpi fursa mwanamke kugombea au kijana au kijana mwanamke ukianza kwa mfano wakati wa uchaguzi kwenda tu kuchukua fomu ni vita.” Amesema Ruge.
Ruge aliongeza kwamba hali hii inawatia hofu vijana na wanawake kutokana na vitisho na utekaji, akisema, “Tunasema tunahamasisha vijana wagombee kuna utekaji kuna mauaji kuna vijana hawajulikani walipo.”
Mzee John Momose Cheyo, Mwenyekiti wa Chama cha UDP, alisisitiza jinsi fedha zinavyohusiana na upatikanaji wa nafasi za kugombea huku akipendekeza kuwa katiba mpya itasaidia kuboresha hali hiyo.
“changamoto ya mwisho ni mfumo wetu wa uchaguzi kwa sababu mhongaji mkubwa ni mgombea sasa kama wewe ndio unataka hizo kura na una hela utapata tu kura na watu wenyewe wanachukua chumvi wengine wanagawana kibiriti kimoja wanahesabiana njiti”, ameeleza mzee Cheyo.
Kwa upande wake Profesa Anna Tibaijuka amesisitiza umuhimu wa kubadilisha mifumo ya ndani ili kutoa nafasi sawa kwa wagombea binafsi. Alisema, “Hauwezi kusema unakwenda kumsimamisha mwanamke kwenye uchaguzi kama wanawake wanabaguliwa kwenye vyama vyao,” na kuongeza kwamba mifumo ya demokrasia inapaswa kuendana na utamaduni wa kitaifa.
Naye Balozi wa Finland, Theres Zitting, alihusisha tatizo la upotoshaji wa habari na changamoto za kidemokrasia akitaka tatizo hilo kushughulikiwa kwa ushirikiano wa mashirika ya kiraia, kampuni za teknolojia, vyama, vyombo vya habari na serikali.
“Wakati haya yote yanapofanya kazi pamoja, nadhani tunaweza kufanikiwa kusonga mbele, kwa sababu kwa kweli ni tishio na uchaguzi ujao, na tunaona kwamba katika nchi nyingi hilo ni suala muhimu”, ameeleza.
Balozi mwingine ni Tone Tinnes wa Norway. Yeye amehimiza umuhimu wa kupiga kura akiwataka watu kujitokeza kupiga kura na kuhamasisha umuhimu wa sauti za wananchi katika uchaguzi.
“Utafiti na masomo yanaonesha kwamba hali ya demokrasia duniani inaporomoka. Ripoti ya Freedom House ya mwaka 2023 inaonesha kwamba demokrasia duniani imeendelea kudorora kwa miaka 18 mfululizo, na Afrika inaongoza kwenye hili. Mwaka ujao kutakuwa na uchaguzi nchini Tanzania kwa ajili ya serikali, na pia kutakuwa na uchaguzi nchini Norway kwa ajili ya bunge na serikali. Ninawahimiza kila mtu kupiga kura, tumia haki yako ya kupiga kura, jiandikishe”, amehimiza Balozi Tinnes.
Hotuba hizi zilimejikita katika kuonesha jinsi changamoto zinavyokwamisha maendeleo ya demokrasia na kutoa mapendekezo ya kuboresha hali hiyo, huku zikisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa na marekebisho ya kisheria na kiutendaji katika mfumo wa uchaguzi.