Askari wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), kwa kushirikiana na Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) na Jeshi la Polisi Wilaya ya Itilima, mkoani Simiyu, wamefanikiwa kumuua fisi aliyekuwa akiwasumbua wakazi wa Kijiji cha Kimali.
Fisi huyo aliyeuawa anadaiwa kuwa na alama ya jina la mtu kwenye paja lake la kushoto na shanga shingoni, hali iliyoibua maswali miongoni mwa wakazi wa eneo hilo.
Mkuu wa Wilaya ya Itilima, Anna Gidarya, akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Mwamigagani, Kata ya Mwalushu, amewataka wote wanaomiliki nyara za serikali kinyume cha sheria kuzisalimisha kwa wahusika wa uhifadhi haraka iwezekanavyo ili kuepuka hatua kali za kisheria.
Kumekuwepo na matukio ya fisi kushambulia wakazi wa Wilaya ya Itilima, hususan watoto, hasa nyakati za usiku kuanzia saa moja. Takwimu zinaonesha kuwa tangu mwaka 2024 hadi sasa, watu nane wamefariki dunia kutokana na mashambulizi ya fisi, huku wengine 17 wakijeruhiwa. Katika kipindi hicho, fisi 16 wameuawa kwa lengo la kudhibiti hatari hiyo.
Mamlaka za uhifadhi zinaendelea kuchukua hatua kuhakikisha usalama wa wananchi katika maeneo yaliyoathirika na mashambulizi ya wanyamapori.