Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Deogratius Ndejembi, amemuelekeza mkazi wa Karatu, Bw. Desderi Damiano, kuendelea na shughuli za maendeleo kwenye viwanja vyake vilivyopo Block ‘J’ baada ya Halmashauri ya Wilaya ya Karatu kushindwa kumlipa fidia kufuatia kutwaliwa kwa eneo lake.
Mhe. Ndejembi alitoa maelekezo hayo alipokuwa akitembelea eneo hilo na kujionea hali halisi, baada ya kusikiliza malalamiko ya wananchi wa Karatu Mjini kwenye Kliniki ya Ardhi iliyofanyika mjini humo Oktoba 5, 2024. Waziri alibaini kuwa Bw. Damiano ameathirika kwa kunyimwa haki ya kuendeleza kiwanja chake kwa muda mrefu kutokana na kutokulipwa fidia.
“Huyu ndiye mmiliki halali wa eneo hili. Hajawahi kulipwa fidia, kwa nini mnamzuia kuendeleza mali yake? Eneo hili ni lake mpaka Halmashauri itakapomlipa fidia. Kwa hiyo, naelekeza aendelee na shughuli zake kama alivyopanga,” alisema Waziri Ndejembi.
Bw. Damiano alizuiliwa kuendeleza viwanja hivyo licha ya Halmashauri kutomlipa fidia, huku eneo hilo likiwa limepangwa kutumika kama eneo la wazi.
Aidha, Waziri Ndejembi alimuelekeza Afisa Ardhi, Joseph Madangi, kutoa maelezo kwa Mkuu wa Wilaya ya Karatu kuhusu jinsi alivyopata Hati ya Miliki ya eneo linalodaiwa kuwa la wazi, huku akimnyima Bw. Damiano haki yake ya umiliki.
Katika hatua nyingine, Waziri Ndejembi alitoa hati za miliki kwa wananchi waliohudhuria Kliniki ya Ardhi iliyofanyika kwenye viwanja vya Mazingira Bora, Karatu, mkoani Arusha.