Serikali ya Iran imetangaza kuwa ipo “karibu sana” kufikia makubaliano na Oman kuhusu mwelekeo mpya wa usafirishaji wa meli katika Njia ya Bahari ya Hormuz, lakini ikatahadharisha kuwa mkataba huo pekee hautatosha kufungua kikamilifu njia hiyo muhimu ya nishati duniani bila Marekani kukubali masharti yake.
Vita hivyo vilivyoanza mnamo Februari 28 kufuatia mashambulizi ya kijeshi ya Marekani na Israel dhidi ya Iranvim efanya Tehran kuweka udhibiti mkali katika njia hiyo inayopitisha takribani robo tano (1/5) ya mafuta na gesi duniani, hatua iliyosababisha mfumuko mkubwa wa bei za nishati na bidhaa duniani.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araqchi, ameeleza kuwa mfumo wa zamani wa usafirishaji wa meli kupitia njia hiyo haukubaliki tena kwa Tehran. Araqchi amebainisha kuwa Iran inazungumza na Oman kuhusu njia ya muda mfupi wakati masuala ya kisheria na kiufundi kuhusu njia ya kudumu yakitafutiwa ufumbuzi.
Hata hivyo, Katibu wa Baraza Kuu la Usalama la Taifa la Iran, Mohammad Baqer Zolqadr, pamoja na Msemaji wa Jeshi la Mapinduzi la Iran (IRGC), Hossein Mohebbi, wameweka wazi kuwa kufunguliwa kwa njia hiyo kunategemea Washington kukubali kupunguzwa au kuondolewa kabisa kwa vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Iran na kuachiwa kwa rasilimali zake zilizoshikiliwa nje ya nchi, Marekani kulipa fidia kwa uharibifu uliotokana na mashambulizi yake nchini Iran, kukomesha vitisho vya kijeshi na kuacha mashambulizi dhidi ya Iran na washirika wake nchini Lebanon, Palestina, Yemen, na Iraq.
“Wakati wowote ambapo Marekani itakubali masharti ya Iran, Njia ya Bahari ya Hormuz itafunguliwa. Hilo halihusiani moja kwa moja na mazungumzo yanayoendelea kati ya Iran na Oman,” amesema Mohebbi.
Wakati mazungumzo hayo yakielezwa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Oman kuwa ni ya “mwelekeo chanya na wa kujenga,” Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) umeripoti kuwa kombora la Iran limepiga meli ya mafuta inayomilikiwa na kampuni ya serikali ya UAE wakati ikipita katika Njia ya Hormuz.
Kituo cha Usimamizi wa Biashara ya Baharini cha Uingereza (UKMTO) kimesema meli hiyo ilipata moto baada ya kushambuliwa, lakini moto huo ulizimwa bila kuleta madhara kwa wafanyakazi au mazingira.
Afisa mmoja wa Serikali ya Marekani ameeleza kuwa Washington inatarajia mkataba kati ya Iran na Oman utafikiwa hivi karibuni, na kwamba pale usafirishaji wa kibiashara utakapofunguliwa bila vizuizi, Marekani nayo itaondoa vikwazo kwenye bandari za Iran.
Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani (CENTCOM) imeeleza kuwa tangu iweke vikwazo hivyo, imeruhusu zaidi ya meli 30 zenye misaada ya kibinadamu kupita, huku ikiwa imezuia meli 53 na kuzikamata nyingine.
Kwa upande wake, Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian ameeleza kuwa hii ndiyo fursa nzuri zaidi ya kufikia makubaliano, akisisitiza kuwa nchi yake ipo kwenye mshikamano mkubwa na kwamba inatoka ikiwa na nguvu katika mzozo huo, ingawa amelaumu vikwazo vya Marekani kwa kupandisha bei za chakula na mahitaji ya msingi nchini humo.