Latest Posts

INEC YACHUKUA HATUA KUJAZA NAFASI ZA MADIWANI KUPITIA VITI MAALUMU

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imetangaza uteuzi wa Madiwani Wanawake wa Viti Maalumu katika halmashauri mbalimbali nchini, hatua inayolenga kujaza nafasi zilizoachwa wazi kufuatia vifo, kuvuliwa uanachama na kujiuzulu kwa baadhi ya madiwani waliokuwepo awali.

Kwa mujibu wa taarifa rasmi ya Tume, uteuzi huo umefanyika baada ya kupokea taarifa kutoka kwa Waziri mwenye dhamana ya Serikali za Mitaa, iliyobainisha uwepo wa nafasi hizo katika halmashauri husika.

Tume imeeleza kuwa ilichukua hatua hiyo kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 57(1) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani, Sura ya 343.

Walioteuliwa katika nafasi hizo ni pamoja na Kalunde Massudi Njiwa atakayehudumu katika Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Agripina Mussa Silodi wa Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe, Syluana Didacus Ndemera wa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya pamoja na Nyamisi Malima Bwire wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda.

Tume imebainisha kuwa uteuzi huo ni sehemu ya kuhakikisha uwakilishi wa wananchi unaendelea bila kuathiriwa na uwepo wa nafasi zilizo wazi, huku ikisisitiza kuwa itaendelea kusimamia mchakato wa kujaza nafasi za uongozi kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizopo.

Hatua hiyo pia inalenga kuimarisha utendaji kazi wa halmashauri husika kwa kuhakikisha kuwa idadi kamili ya madiwani inapatikana ili kutekeleza majukumu ya maendeleo na utoaji wa huduma kwa wananchi kwa ufanisi zaidi.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!