Latest Posts

KAMISHENI YA BONDE LA ZIWA VICTORIA YAJADILI MATUMIZI YA LUGHA RAHISI KATIKA UHIFADHI WA BONDE LA MARA

Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria imeanza kujadili njia bora za kutumia lugha rahisi na zinazoeleweka kwa jamii zinazozunguka Bonde la Mto Mara ili kuleta matokeo bora katika uhifadhi wa rasilimali za bonde hilo.

Kauli hiyo imetolewa na Dkt. Masinde Bwire, Katibu Mtendaji wa Kamisheni hiyo, katika kongamano la kisayansi lililofanyika katika Chuo Kikuu cha Masai Mara, Kaunti ya Narok, Kenya.

Dkt. Bwire ameeleza kuwa moja ya changamoto zinazokabili juhudi za uhifadhi ni jamii kutokuelewa lugha ngumu zinazotumika katika tafiti mbalimbali.

“Tunachukua jukumu la kuhakikisha kwamba tafiti zetu zinatafsiriwa kwa lugha rahisi inayoeleweka na jamii. Hii itasaidia katika ulinzi wa rasilimali na kuwapa uwezo wanajamii kushiriki kikamilifu katika uhifadhi,” amesema Dkt. Bwire.

Pia amesisitiza umuhimu wa kutumia lugha zinazofanana na jamii zinazozunguka bonde hilo ili kurahisisha mawasiliano na kuongeza uelewa juu ya umuhimu wa kulinda rasilimali za Ziwa Victoria.

Kwa upande wake, mwanazuoni maarufu Profesa Patrick Lumumba ameeleza kuwa matokeo mengi ya tafiti yameandikwa kwa lugha ngumu na hazieleweki kwa watu wa kawaida.

“Tunapaswa kutumia maneno rahisi na misamiati inayoeleweka na jamii husika ili kuwapa nafasi ya kuelewa na kuchukua hatua za kulinda mazingira. Tafsiri sahihi ni muhimu ili kuondoa maneno magumu kama ‘ikolojia’ na ‘baianua’ ambayo hayaeleweki kirahisi kwa wanajamii.” Alisema.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanal Evans Mtambi amehimiza kila mwananchi kutambua jukumu lake katika kulinda mazingira na wanyama wanaopatikana katika bonde hilo, akisisitiza kwamba ushirikiano wa jamii ni muhimu katika juhudi za uhifadhi.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!