Na Josea Sinkala, Mbeya.
Mchungaji na mwimbaji wa nyimbo za injili nchini Tanzania Alex Mahenge, ametangaza kuwania nafasi ya Rais wa Jamuhuri ya muungano wa Tanzania mwaka 2030 akidai kubadilisha maisha ya wa-Tanzania kwasababu wao ni matajiri.
Mahenge, amesema hayo kwenye mahojiano yake maalumu kuhusu azma yake ya kuwa Rais wa Tanzania na anavyoona mwenendo wa nchi na maendeleo yaliyofikiwa katika awamu hii ya sita ndani ya miaka 63 ya uhuru.
Amesema ni jambo la aibu kuona mpaka sasa viongozi mbalimbali wakiwemo mawaziri wanahimiza ujenzi wa vyoo ili kutokomeza kipindupindu katika zama hizi.
Alipoulizwa sababu za hadi sasa kuonekana ujenzi wa vyoo ukihimizwa na kupambana na kipindupindu alijibu ‘Tumechelewa, hili ni jambo la aibu yaani mimi kama Waziri au Rais wa nchi nawambia watu wajenge vyoo, tumechelewa sana na nchi yetu ni tajiri shida tumekaa tu kwenye kukaririshwa kuwa ni masikini lakini sisi ni matajiri kwani tuna raslimali nyingi kama madini, bahari, misitu, kilimo, mito na maziwa, mbuga za wanyama na mengineyo”.
Hata hivyo Alex Mahenge ambaye kwa sasa ni kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) amesema angekuwa amejipanga vizuri angegombea urais wa Tanzania lakini pia kutokana na mfumo wa CCM anaamini Mungu atamjalia kuwania nafasi hiyo mwaka 2030.
Ameeleza kuwa endapo atachaguliwa kuwa Rais wa nchi atahakikisha anaondoa kero mbalimbali zinazowakabili wananchi hasa utitiri wa kodi na tozo mbalimbali ikiwemo kwenye magari ambayo yananunuliwa kwa bei ndogo nje ya nchi lakini hadi kumfikia mtanzania ni gharama kubwa kutokana na ukubwa wa kodi.
“Wananchi hawana furaha, yaani wa-Tanzania tunaishi kwa manyanyaso, yaani mtanzania ukikutana na daktari nikama umekutana na mwanajeshi, akikutana na mwanajeshi nikama amekutana na gaidi, akikutana na mwalimu nikama amekutana na Polisi yaani mtanzania kila anapoenda ni manyanyaso yaani unaweza kutoka nyumbani kwako kwenda mgahawani na ukafika na kujibiwa juu juu tu!”, ameeleza Alex Mahenge mwimbaji wa nyimbo za injili na Mchungaji katika kanisa la Evangelical assemblies of God Tanzania (EAGT).