Ikiwa ni Novemba 5, 2024 Wamarekani wanajitokeza kupiga kura kuchagua rais ajaye wa taifa lao, lakini matokeo ya kura za umma nchini kote hayatoamua mshindi moja kwa moja. Badala yake, uchaguzi wa rais nchini Marekani unategemea mfumo wa Electoral College, ambapo wajumbe ndiyo wanaotoa uamuzi wa mwisho.
Electoral College ni mfumo uliowekwa na waanzilishi wa Marekani mwaka 1787 ili kuleta usawa wa uwakilishi wa majimbo na kuzuia wagombea wasiofaa kushika madaraka. Katika mfumo huu, kuna wajumbe 538 kutoka majimbo yote 50, ambapo idadi ya wajumbe kwa kila jimbo inategemea uwakilishi wa jimbo hilo bungeni. California, kwa mfano, ina wajumbe 54 kutokana na idadi yake kubwa ya watu, huku Wyoming ikiwa na wajumbe watatu tu.
Mgombea wa urais anahitaji angalau kura 270 za wajumbe kati ya 538 ili kuibuka mshindi. Majimbo mengi yanafuata utaratibu wa “mshindi kuchukua yote,” ambapo mgombea anayeongoza katika kura za umma kwenye jimbo fulani anapata kura zote za wajumbe wa jimbo hilo. Hata hivyo, Maine na Nebraska hugawa kura za wajumbe kulingana na matokeo ya kila wilaya ya uchaguzi.
Pamoja na mfumo huu, kuna uwezekano wa rais kushinda urais hata bila kuwa na kura nyingi za umma kitaifa. Hii imetokea mara tano katika historia, ikiwa ni pamoja na uchaguzi wa mwaka 2016 ambapo Donald Trump alipata kura chache kuliko Hillary Clinton, lakini aliibuka mshindi. Mfumo wa Electoral College umekosolewa kwa muda mrefu na kuna zaidi ya mapendekezo 700 ya kuufanyia marekebisho au kuufuta kabisa, ingawa hakuna hata moja lililopitishwa.
Licha ya kuwa na taratibu maalum zilizoandikwa kwenye Katiba, wajumbe hawalazimiki kupiga kura kulingana na matokeo ya wapiga kura wa jimbo lao. Katika historia ya Marekani, wajumbe 90 walipiga kura kwa mgombea tofauti na chaguo la wananchi, japo matukio haya ni nadra na si mara nyingi huathiri matokeo ya uchaguzi.