Na; John Marwa
Siku chache kabla ya siku ya uteuzi wa wagombea wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Makamu Mwenyekiti Tanzania Bara wa chama kikuu cha upinzani nchini yaani Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Tundu Lissu alinukuliwa akisema kuwa chama hicho kinakabiliwa na changamoto ya wagombea katika uchaguzi unaoendelea wa serikali za mitaa
Lakini kama hiyo haitoshi, licha ya tambo zao na kujipiga kifua viongozi wa ACT Wazalendo sirini nao pia wanakiri kuwa hawana wagombea wa kutosha katika uchaguzi huu, hiyo ndio sawa na kusema kwamba ushindani wa vyama vya upinzani kwa chama tawala yaani Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa namna yoyote ile kwenye uchaguzi huu haiwezi kulandana kwa kuwa kitendo cha kuwa na wagombea wachache tu ni dhahiri kuwa kinatoa mianya ya CCM kukosa ushindani kwenye maeneo mengi jambo ambalo ni faida kwao kama chama tawala
Jambo Online TV imefanya uchunguzi wake kwa kutumia sampuli ya baadhi ya maeneo ya nchi kwa kuzungumza na viongozi wa vyama tofauti vya siasa kuanzia CCM, CHADEMA, ACT Wazalendo, CUF nk sambamba na wasimamizi wa uchaguzi, ambapo matokeo ya uchunguzi huo kwa kiasi kikubwa yanashabihiana kabisa na kile kilichosemwa hadharani na Tundu Lissu, na kile wanachokiri sirini baadhi ya viongozi wa ACT Wazalendo
Kwa mfano, wakati Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Pwani Boniface Jacob (Boni Yai) alipokutanisha wagombea wa chama hicho mkoa wa Dar es Salaam alieleza kuwa CHADEMA ina wagombea 95% ya mitaa yote ya jiji la Dar es Salaam, lakini uchunguzi wetu umeonyesha kuwa ilikuwa ni tambo za siasa tu, ndio tuna ujasiri wa kusema tambo za siasa kwa kuwa jimbo la Kigamboni kwa mfano chama hicho kimeweka wagombea chini ya nusu ya mitaa yote, kata ya Manzese katika jimbo analotoka Boni Yai mwenyewe yaani Ubungo yenye mitaa 10 CHADEMA ina wagombea mitaa mitano (5) tu, na katika jimbo la Kawe hususani mtaa wa Masaki chama hicho hakina hata mgombea wa ujumbe wa kamati ya mtaa
Hayo ni tofauti na taarifa zilizotolewa na viongozi wa CHADEMA Kanda ya Pwani, kwani kwa mujibu wa katibu wa kanda hiyo Jerry Kerenge alidai kuwa katika mkoa wa Dar es Salaam wenye mitaa 564, CHADEMA ilikuwa imesimamisha wagombea kwenye mitaa 547 ambapo ni sawa na asilimia 95 ya mitaa yote
Hali ni hiyo hiyo kwa Chama cha ACT Wazalendo, ambacho bila kumung’unya maneno hiki ndicho chama cha pili kwa ukubwa katika vyama vya upinzani hapa nchini, majimbo ya Temeke na Mbagala ambayo ni majimbo ya hakika ya chama hicho wagombea wa chama hicho ni 30% tu ya mitaa yote inayogombewa
Hali ni mbaya zaidi kwenye majimbo ya vijijini na mikoa ya pembezoni kwa vyama vyote 2 vikuu vya upinzani hapa nchini, na hapa nieleweke kuwa natambua mchango na nafasi ya vyama vingine vya upinzani nje ya CHADEMA na ACT Wazalendo lakini kila mmoja atakubaliana nami kuwa kama tunataka kuona au kujadili taswira ya upinzani nchini ni lazima macho na masikio yetu yajielekeze kwenye vyama hivyo viwili (2)
Licha ya ‘udhaifu’ huo wa vyama vya upinzani nilioueleza kwa uchache hapo juu lakini kilichotokea siku ya uteuzi tarehe 8/11/2024 ni kama imewapa nguvu vyama hivi viwili (2), kitendo cha wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi kuwaengua wagombea wa upinzani licha ya uchache wao kumewapa nguvu ya kueneza propaganda ya vyama hivi kiasi cha kuficha udhaifu wao wa kutokuwa na wagombea
Hata bila kuwaengua wagombea wao tayari CCM walikuwa wanabaki peke yao kwenye 70-75% ya vitongoji, vijiji na mitaa yote ya Tanzania Bara ambako uchaguzi huo ndiko unakofanyika, kwenye nafasi ya Wenyeviti wa vitongoji, vijiji na wajumbe wa Halmashauri ya kijiji CCM inagombea peke yake katika zaidi ya 80% ya nafasi hizo, vivyo hivyo kwenye mitaa
Sasa swali la kujiuliza hapa, kwa nini mfumo unavumilia vitendo vya wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi kama hali ni hii?, mfumo hauoni kuwa unawapa wapinzani wao sifa ambazo hawana na wakati huo huo kujiharibia ushindi wa halali kabisa kwa chama tawala (CCM)?
Maeneo kama Hai, Kigoma mjini, Tunduru Kaskazini, Tunduru Kusini na Arusha mjini ni maeneo yanayojulikana wazi kuwa ni ngome za upinzani, na ndio maeneo pekee ambayo wapinzani wamejitahidi kuweka wagombea wengi, huku nako wagombea wao wamekatwa katwa kwa sababu ambazo ukiziangalia hazina maana kabisa, dola haioni kuwa inajichafulia yenyewe taswira ya uchaguzi huu?
Nimepita kwenye maeneo tofauti na kufuatilia maeneo mengine ili kujuwa sababu zilizopelekea wagombea hao kuenguliwa, kwa kiasi kikubwa wengi wao kama sio wote wameenguliwa kwa sababu kama vile wagombea hawajajiandikisha kwenye daftari la mkazi, hawana shughuli au kazi za kuwaingizia kipato, hawana udhamini wa chama, sio wakazi wa maeneo husika, wamekosea kuandika majina ya vitongoji, vijiji au mitaa (na hapo kuna suala la kuongezwa kwa herufi nk), lakini ipo sababu nyingine ya kwamba majina ya kwenye fomu iliyojazwa na mgombea hayafanani na majina ya kwenye daftari la mkaazi (hapa kuna wagombea wameongezea herufi au kuhariri nk), kubwa kuliko yote wapo walioenguliwa kwa sababu tu hawajakidhi vigezo bila kuainishwa ni vigezo vipi ambavyo hawajakidhi
Hili limenifanya nirejee kanuni za msingi na za lazima za uchaguzi wa serikali za mitaa nikaona miongoni mwake ni kwamba ni lazima awe raia wa Tanzania, awe na umri wa kuanzia miaka 21 au zaidi, awe na uwezo wa kujuwa kusoma na kuandika kiswahili au kiingereza, awe na shughuli halali ya kumuwezesha kuishi, awe mkazi wa eneo la kitongoji, kijiji au mtaa husika, awe mwanachama wa chama cha siasa na awe amedhaminiwa na chama hicho, lakini pia awe na akili timamu
Kama hizo ndio kanuni za msingi wale wanalioenguliwa kwa kigezo eti mgombea au wagombea husika hawajajiandikisha kwenye daftari la mkaazi wametoa wapi kanuni hiyo?, lakini hata ukizungumzia shughuli au kazi halali ya mtu unaipimaje ili ukubali kuwa hii ni kazi halali?
Nimemsikiliza hivi karibuni Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya nje wa CHADEMA John Mrema akidai kuwa baadhi ya wagombea wao wameenguliwa kwa kigezo hicho, tutolee mfano jiji kama la Dar es Salaam kuna wajasiriamali wadogo wadogo kabisa kama vile wauza karanga, uji, maji, juisi, nk hawa wakiamua kugombea ni kweli wanastahili kuenguliwa?
Nimewahi pia kumsikia Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila akikiri wazi kuwa mkoa anaouongoza idadi kubwa ya watu wanaamka wakiwa hawajuwi watakula nini, na pengine wanaamka wanahangaika wanapata hela ya chai, kisha wanahangaika tena wanakula chakula cha mchana au usiku kisha wanalala wanasubiri kesho, hiyo haimaanishi kuwa hawafanyi kazi halali bali kazi wanazofanya na vipato vyao havishabihiani kwa hiyo binafsi sidhani kama ni sawa mtu kama huyu kumuengua pale anapotaka kugombea
Nikiendelea kupitia sababu kadha wa kadha ambazo zimetumika kuenguliwa kwa wagombea wa upinzani nimekutana na malalamiko ya Wakili Deogratias Cosmas Mahinyila ambaye naye aligombea nafasi ya Mwenyekiti wa kijiji cha Berege, kilichopo Mpwapwa, mkoani Dodoma ambapo yeye ameambiwa kuwa si mkazi halisi wa eneo lile
Wakili Mahinyila alikuwa mgombea wa nafasi ya Udiwani katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 akipeperusha bendera ya CHADEMA kwenye kata ya Berege, inawezekanaje mtu ambaye si mkazi akakubaliwa mwaka 2020 na kugomewa 2019?, licha ya kwamba ni chaguzi mbili tofauti lakini msingi wa hoja yangu hapa ni kwamba mtu huwa anagombea kwenye eneo ambalo ana uhakika nalo yaani analofahamika
Kam hiyo haitoshi Wakili Mahinyila ameorodheshwa kwenye daftari la mkazi katika kijiji cha Berege, na hakuna pingamizi lolote dhidi yake kuwa yeye si mkazi wa eneo lile kwa nini akose sifa za kugombea, yaani ana sifa za kuchagua lakini hana sifa za kuchaguliwa?
Naweza kumuelewa msimamizi msaidizi wa uchaguzi pengine labda anaona Wakili Mahinyila anaingia na kutoka mara kwa mara kijijini hapo, lakini inaeleweka wazi kuwa kazi kubwa anayoitegemea imuingizie kipato ni Uwakili wake na bila shaka idadi kubwa ya wateja wake wako nje ya Berege, sasa je pale anapopata kazi nje ya eneo hilo asiende?, haya yote ni maswali yanayotengenezwa kutokana na wagombea wa upinzani kuenguliwa kwa ‘uonevu’
Wilaya ya Mpwapwa ni sehemu ya mkoa wa Dodoma, mkoa ambao hakuna asiyefahamu kwamba kwa miaka yote hiyo imekuwa miongoni mwa ngome imara za CCM, kwa nini maeneo kama haya pale inapotokea wapinzani wachache wamejitokeza wasiachwe tu wafike hadi kwenye debe?, na pengine angalau wangetumika kama kichaka?, hofu hii ya watawala/dola inatokana na nini?
Jambo Online TV imeshikwa na butwaa na yanayoendelea, ukweli ni kwamba Tanzania inachafuka, CCM wanakosa uhalali wa ushindi wao wa ukweli na wapinzani wanapata kichaka cha kuficha udhaifu wao kitu ambacho hakisaidii Taifa letu.