Na Mwajuma Hassan, Iringa
Maboresho ya Sera ya Taifa ya Ardhi ya mwaka 1995, kupitia toleo jipya la mwaka 2023, yameanza kuleta mabadiliko chanya kwa wananchi wa kawaida, hasa katika kurasimisha makazi na kumaliza migogoro ya ardhi iliyodumu kwa miaka mingi.
Hali hiyo imejidhihirisha katika Kata ya Isakalilo, Manispaa ya Iringa, ambako jumla ya wananchi 267 wamekabidhiwa hatimiliki za ardhi, hatua inayotajwa kuwa ni suluhisho muhimu kwa changamoto za muda mrefu zinazohusu umiliki halali wa ardhi.
Katika hafla hiyo ya kihistoria, wakazi wa eneo hilo walionyesha furaha kubwa, hasa wazee ambao kwa muda mrefu wameishi bila nyaraka za kumiliki ardhi wanayoishi.
Miongoni mwa walionufaika ni Bibi Anyesi Nyilowa mwenye umri wa miaka zaidi ya sabini ambaye baada ya miongo saba ya kuishi bila hati, sasa ametambuliwa rasmi kama mmiliki halali wa ardhi hiyo.

“Tulijua tutakufa tu bila kupata hati hii, lakini sasa wajukuu zetu watapata kitu cha maana katika maisha yao,” alisema kwa hisia Bibi Anyesi.
Mumewe, Mzee Musa Sangwa, alisimulia maisha ya nyuma yaliyokosa uelewa kuhusu haki ya umiliki wa ardhi.
“Mimi sikuwa najua kama kuna haki ya kumiliki ardhi. Tulikuwa tunagawana tu na wenzetu, lakini leo nimepata hati hii,” alisema kwa furaha.
Wanandoa hao ni mfano hai wa mafanikio ya utekelezaji wa sera mpya ya ardhi ambayo inalenga kuondoa urasimu katika utoaji wa hatimiliki na kuweka mazingira bora ya usalama wa miliki pamoja na kuinua maisha ya wananchi kiuchumi.

Devotha Kimota, mmoja wa walionufaika, alisema kuwa hati hiyo itamuwezesha kupata mikopo kwa ajili ya kukuza shughuli zake za kiuchumi.
“Nimefurahi sana kupata hati hii, kwa kuwa itanipa fursa hata ya kukopa katika taasisi mbalimbali,” alisema.
Kwa upande wake, Afisa Ardhi Mteule wa Manispaa ya Iringa, Zera Chaula, alieleza kuwa zoezi hilo ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa serikali wa kupunguza migogoro ya ardhi nchini.
“Manispaa ya Iringa imepangiwa kuandaa hati 2,500, lakini bado hatujafikia lengo. Tunahitaji kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kurasimisha maeneo yao,” alisema.
Hata hivyo, Afisa huyo alikiri kuwa bado kuna changamoto ya uelewa mdogo kuhusu sera mpya miongoni mwa wananchi, hali inayohitaji juhudi zaidi katika utoaji wa elimu kupitia vyombo vya habari na mikutano ya hadhara.
Katika kusaidia juhudi hizo, Shirika la Kimataifa la Landesa linalojihusisha na masuala ya ardhi, limeanza kutoa mafunzo kwa waandishi wa habari nchini ili kuwawezesha kusaidia jamii kuelewa kwa kina mabadiliko hayo.
“Ardhi ni hatima. Kile mtakachoandika kuhusu masuala ya ardhi kinaweza kujenga hatima ya kizazi cha sasa na baadaye,” alisema Queen Mrema, mwakilishi wa Mkurugenzi wa Landesa Tanzania.
Naye mtaalamu wa ardhi kutoka Landesa, Masalu Luhula alisema kuwa sera mpya inasisitiza usawa wa kijinsia na utatuzi wa migogoro ya ardhi kwa njia shirikishi na ya amani.

“Sera hii imeweka wazi kuwa kutakuwa na mabadiliko makubwa katika mifumo ya utatuzi wa migogoro ya ardhi. Waandishi wa habari wana nafasi muhimu ya kuielimisha jamii kuhusu mabadiliko haya,” alibainisha.
Mwandishi mkongwe, Deodatus Mfugale, aliwahimiza waandishi wa habari kutumia taaluma yao kuchambua sera hiyo kwa kina na kutoa taarifa zenye kueleweka kwa jamii.
“Waandishi wa habari waichambue sera, wajue tatizo ni nini, sera inasema nini, na wananchi watanufaika vipi,” alisema Mfugale.
Kupitia maboresho haya ya sera, serikali inalenga si tu kumaliza migogoro ya ardhi baina ya wakulima, wafugaji, wawekezaji na familia, bali pia kuimarisha maisha ya wananchi na kukuza uchumi wa taifa kwa kuweka misingi imara ya haki ya miliki ya ardhi.