Latest Posts

MADAI YA RUSHWA NDANI YA CHADEMA NA HISIA MSETO ZA WADAU

Kwa muda mrefu sasa kumekuwa na minong’ono na maneno ya hapa na pale kuhusiana na madai ya uwepo wa harufu ya rushwa ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ambapo minong’ono hiyo imekuwa ikijieleza kuwa huenda mdudu huyo wa rushwa amekuwa akikitafuna chama hicho kuanzia ngazi ya chini hadi juu kabisa kwa maana ngazi ya Taifa

Mara zote ambazo madai hayo yanapotolewa, iwe kutoka kwenye vyanzo vya ndani au nje ya CHADEMA lakini kwa kiasi fulani yamekuwa yakikosa nguvu ya ushawishi wa kutengeneza mjadala wa kina, na hiyo ilitokana na ukweli kwamba viongozi, wanachama na baadhi ya wafuasi wa chama hicho wamekuwa mstari wa mbele kutoa kauli za kukanusha madai hayo, inawezekana wanakanusha kwa maana ya kukanusha kweli kwamba kitu hicho hakipo lakini upande wa pili inawezekana wanakanusha kwa maana ya kutafuta njia ya kukilinda chama tu lakini uhalisia wanaujuwa kuwa yaliyomo yamo, yote kwa yote wao wanaweza kuwa waelewa zaidi kwenye suala hilo

Wakati mjadala wa jambo hilo ukiingia na kutoka, hivi karibuni moto wake ulikolezwa zaidi baada ya mmoja wa viongozi wa juu kabisa wa chama hicho kuibua na kueleza tuhuma nzito zinazohusiana na rushwa ndani ya CHADEMA

Alikuwa ni Tundu Lissu ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Tanzania Bara ambaye mara kadhaa alitumia majukwaa mbalimbali ya mikutano ya hadhara na hata mahojiano na vyombo vya habari kueleza kuhusu madai ya uwepo wa rushwa ndani ya chama hicho

Ingawa mara zote haijawahi kuibuka na kutaja wahusika moja kwa moja kwa majina yao, lakini Lissu ambaye pia alikuwa mpeperusha bendera wa CHADEMA kwa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 lakini ameonesha kukerwa na kile alichodai kuwa uwepo wa ‘fedha chafu’ ndani ya chama hicho

Kauli ya mtu wa kariba ya Lissu, tena anayoitoa kwa kukosoa chama chake kabisa na ikizingatiwa kuwa kwa ukubwa wake aliitoa akiwa kwenye mkutano wa hadhara wa chama hicho mkoani Iringa ikiwa ni siku chache kabla ya uchaguzi wa CHADEMA Kanda ya Nyasa, inatafakarisha sana

Ndio, katika maelezo yake alidai kuwa mwanzoni alipewa ushauri kuwa asitembelee Kanda hiyo hadi pale watakapomaliza uchaguzi huo lakini yeye anasema alilazimika kwenda ili akaongee ukweli kabla ya uchaguzi ili mambo yasiharibike zaidi, sina hakika kama kauli yake ilipelekea ‘fedha chafu’ alizozitaja kuondoka au ndio ilichochea zikaendelea kufanya kazi, ninachoweza kusema bila wasiwasi ni kwamba kauli yake ilikoleza moto wa mjadala kuhusu harufu ya rushwa ndani ya CHADEMA

 

Kabla, wakati na hata baada ya uchaguzi wa CHADEMA Kanda ya Nyasa mjadala kuhusu rushwa ulipamba moto zaidi ikidaiwa kuwa hata michakato ya uchaguzi kuanzia ngazi za chini za msingi, kata, jimbo, mkoa hadi Kanda imegubikwa na rushwa, huku madai hayo yakienda mbali zaidi kuwa pengine baadhi ya vigogo ngazi ya Taifa wamehusika kwa namna moja au nyingine, hiyo ilibaki hivyo na inaendelea kubaki hivyo

 

Wakati kombe la mwanaharamu tukijuwa limeshafunikwa na sasa maisha mengine yakichukua nafasi yake, kwenye Kanda hiyohiyo ya Nyasa linaibuka jipya, jipya si kwa maana ya jipya masikioni la hasha, bali upya wake ni kwa sababu linasikika kwa mara ya kwanza lakini kwa wafuatiliaji wa mambo hawawezi kuliona jipya kwa sababu wanakumbuka kauli za Lissu alizotoa akiwa Iringa, wanakumbuka mazingaombwe wa chaguzi za CHADEMA kwa ngazi mbalimbali Kanda ya Nyasa wanaona kuwa yanayotokea sasa ni muendelezo wa hayo

 

Mimi ni mfuasi hasa wa mitandao ya kijamii, naweza kusema mijadala mingi inayoanzia, kuibuliwa au kujadiliwa huko nimekuwa nikikutananayo na pengine kushiriki (iwe ya siasa, jamii, uchumi, michezo, sanaa na hata burudani), ingawa kwa kiasi kikubwa nimekuwa mfuatiliaji wa mijadala ya siasa, jamii na uchumi

 

Hivi karibuni kupitia mitandao hiyo nimeona na kusikia sauti ya dada mmoja ambaye jina lake sijalikamata mara moja akiwa anaeleza na kusimulia kwa kujiamini kabisa jinsi mtu mmoja anayeitwa Sam ambaye kwa maelezo yake anadai ni wa Chama cha Mapinduzi (CCM) alivyowapa hela baadhi ya viongozi, wanachama na wafuasi wa CHADEMA hususani wale wenye sifa za kupiga kura ndani ya chama hicho yeye akiwemo, ili tu wafanye kazi ya kumuangusha Rose Mayemba aliyekuwa anagombea nafasi ya Mwenyekiti wa CHADEMA mkoa wa Njombe, ambao ni sehemu ya mikoa inayounda Kanda ya Nyasa, na kwa wafuatiliaji wenzangu wa siasa mtakumbuka sarakasi za uchaguzi wa mkoa wa Njombe zilivyokua

Kama hiyo haitoshi, hisia mseto zimetamalaki miongoni mwa wadau wa siasa hususani wale wanaoamini kwenye hoja na sera za CHADEMA ambapo wengi wao baada ya kumsikiliza dada huyo wameoneshwa kukerwa, kukasirishwa lakini kubwa kuliko yote kuumizwa hali iliyopelekea kuhoji, kama CHADEMA kweli inashiriki vita vya kuiondoa CCM kama chama tawala kwa kigezo kuwa ndani ya chama hicho na serikali kuna mianya ya rushwa

Sauti ya Watanzania, ni jukwaa linalokutanisha Watanzania wengi walioko kwenye kila kona Dunia kote, mijadala mbalimbali chechemuzi imekuwa ikichukua nafasi yake huko bila woga, kificho, au kuoneana haya, niwe mkweli hapa kueleza hisia zangu kuwa nimekuwa mfuatiliaji na kufurahishwa na mijadala ile kwani kwa kiasi kikubwa imekuwa ikiangazia masuala mbalimbali yanayohusu nchi yetu

Mjadala wa rushwa ndani ya CHADEMA nao haujaachwa salama hata kidogo, umechukua nafasi yake hasa na kwa kiasi kikubwa wengi wameinyooshea kidole chama hicho kikuu cha upinzani nchini kwa kile kinachoendelea

Nimemsikiliza mmoja wa wachangiaji wa mjadala ule anayefahamika kwa jina la Mzee Fumbuamacho, najuwa kwa sasa hayuko hapa nchini lakini kwa kiasi kikubwa ameichambua CHADEMA kwa matandu na makoko haswaa

Katika hoja zake ameenda mbali zaidi kuwa huenda CHADEMA kama chama cha siasa chenye wafuasi wengi na chama kikuu cha upinzani nchini hakiko tayari kuchukua hatamu ya kuongoza Tanzania kutokana na kile alichodai kuwa ni jambo ambalo halikubaliki kuona chama kinachopiga kelele, kukosoa sera na mipango ya chama tawala (CCM) na hasa kuahidi kupambana na masuala ya rushwa na ufisadi endapo kitashika dola lakini leo ndani ya chama hicho viongozi, wanachama na wafuasi wanatuhumiana mikono yao kupokea au kutoa rushwa

Katika maelezo yake ni kama vile ametumia msemo wa ‘heri nusu shari kuliko shari kamili’, kwani Mzee Fumbuamacho anadai kuwa haoni umuhimu wa kupiga kelele za kuing’oa CCM madarakani kwa sababu ambazo yule anayetarajia ashike madaraka anazifanya sasa akiwa huko nje ya madaraka jambo ambalo hatarishi

Ameenda mbali zaidi kwa kumuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan pengine ampe nafasi ndogo tu ya kuwa na uwanja wa kuitumikia CCM au nchi kwa namna yoyote ile lakini kwa njia itakayomkutanisha watu ili atumie jukwaa hilo kumnadi yeye (Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan), sambamba na kuhakikisha anamshauri namna ya kushughulikia wahuni, wala rushwa, wezi, mafisadi na wazembe walioko ndani ya CCM, serikali na kwingineko akiwa ndani ya CCM

Siko hapa kueleza kuwa naungana na msimamo wake au la, lakini nipo hapa kuongeza uchechemuzi wa mjadala huu ulioota mizizi kuhusu madai ya rushwa ndani ya CHADEMA.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!