Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Mji Nanyamba mkoani Mtwara limetakiwa kuhakikisha linasimamia ukusanyaji wa mapato kikamilifu kama ambavyo walidhimiria.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Tawala mkoa wa Mtwara, Robert Musungwi amesema mwenendo wa ukusanyaji wa mapato katika Halmashauri hiyo hauridhishi kutokana na kutofikia malengo ya ukusanyaji waliojiwekea ambapo kwa bajeti ya robo mwaka 2024/2025 ilitakiwa kukusanywa shilingi milioni 607 badala yake wamekusanya shilingi milioni 231 pekee.
“Posi sio changamoto inayopelekea kukwamisha maendeleo kwasababu lipo ndani ya uwezo wa halmashauri hiyo.”Amesema Musungwi
“Mwenyekiti taarifa nyingi za kata zinasema changamoto ni posi, kwa nini posi iwe changamoto, cha msingi tuainishe posi ngapi zinahitajika ili tusijadili tena kwenye kikao tuje na mpango mkakati sababu lipo ndani ya uwezo wa halmashauri.”Amesema Musungwi
Hata hivyo Mwenyekiti wa baraza hilo Jamali Kapende amesema kuwa kukosekana kwa posi ni changamoto kubwa sababu wananchi wengi hawakubali kulipa malipo ya serikali bila ya kuwa na uthibitisho ingawa tayari wameshaweka mpango mkakati ili kuhakikisha sehemu zote zenye upungufu wa posi zinapatikana.
Ameongeza kuwa posi moja inagharimu fedha za kitanzania shilingi 500,000 ambapo kabla ya kununuliwa lazima wapate kibali kutoka serikalini ili ukusanyaji wa mapato uonekane kwenye mfumo.
Ikiwa ni kikao cha kwanza cha robo mwaka 2024,2025 cha baraza la Madiwani wa halmashauri ya Mji Nanyamba mkoani Mtwara ukosefu wa posi itumikayo kutolea risiti ya kukusanyia mapato kwa wananchi imeibuliwa kuwa ni changamoto kubwa inayopelekea baadhi ya vijiji kushindwa kabisa kukusanya mapato kwa ajili ya maendeleo ya halmashauri hiyo.