Latest Posts

MAGUTA YA UMEME YAPATA NGUVU MPYA: SERIKALI YASIKILIZA, MAFUNZO YATOLEWA

Serikali imepunguza gharama za leseni kwa madereva wa bodaboda, bajaji na maguta ya umeme kutoka shilingi 100,000 hadi 30,000 katika bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026, hatua ambayo imepongezwa kama ishara ya usikivu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, wakati wa kufunga mafunzo ya madereva wa maguta ya umeme yaliyofanyika katika Chuo cha Polisi jijini Dar es Salaam, mwezi mmoja tu tangu atoe wito wa kuhakikisha wasafirishaji hao wanasajiliwa rasmi.

“Usemi wa ‘ombeni nanyi mtapewa’ sasa umeonekana kwa vitendo. Rais Samia amesikiliza kilio chenu na leo tunashuhudia vijana wakipata mafunzo, leseni, na usajili wa TRA na LATRA,” alisema Mpogolo mbele ya wahitimu na viongozi wa Jeshi la Polisi.

Mafunzo hayo yaliwalenga madereva wa maguta ya umeme kutoka maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam, lengo likiwa ni kuwajengea uwezo wa kitaaluma na kuwapatia nyenzo za kufanya kazi kwa ufanisi na kwa kufuata sheria.

Mpogolo amesema serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwa vijana hao, huku akisisitiza umuhimu wa kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kuepuka ajali na msongamano, hasa katika maeneo ya masoko na katikati ya jiji.

Mkuu huyo wa wilaya pia alitoa onyo kwa watakaokaidi sheria, hasa wale watakaoziba njia au kufanya kazi bila mpangilio, akisema hatua zitachukuliwa kwa yeyote atakayeharibu taswira ya mfumo huo mpya wa usafirishaji kwa nishati safi.

Katika hatua nyingine, madereva hao waliiomba serikali kusaidia kushusha bei ya maguta, betri, na kutenga maeneo rasmi ya maegesho. Mpogolo aliahidi kufikisha maombi hayo kwa Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Elihuruma Mabelya, huku akitoa rai kwa vijana hao kujiunga katika vikundi vya SACCOS na kuomba mikopo ili kujiinua kiuchumi.

Jeshi la Polisi lilitambuliwa kwa mchango wake wa kutoa mafunzo hayo kwa punguzo kubwa kutoka shilingi 100,000 hadi 40,000. Kwa upande mwingine, TRA na LATRA zimesajili na kutoa leseni kwa madereva hao ili kufanya kazi kwa uhalali na amani barabarani.

Mpogolo pia amesema serikali ipo kwenye mazungumzo na kampuni zinazotengeneza maguta ya umeme ili zije kuwekeza nchini, hatua itakayosaidia kudhibiti bei ya vipuri na kuondoa madalali.

Mafunzo hayo yalihitimishwa kwa madereva wote kupatiwa vyeti, leseni na kuahidi kuwa mabalozi wa nidhamu barabarani, huku wakihamasisha vijana wengine kujiunga ili kupunguza changamoto za usafirishaji wa mizigo kwa haraka.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!