Latest Posts

MAHAKAMA YACHELEWESHA UAMUZI WA KESI YA OLENGURUMWA KWA MARA YA TANO

Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) umelaani vikali ucheleweshaji wa kusomwa kwa uamuzi mdogo wa Mahakama Kuu katika kesi ya Wakili Onesmo Olengurumwa (Wakili), Mratibu wa Kitaifa wa THRDC dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
 
Kesi hiyo ambayo imeendelea kuahirishwa tangu Novemba 28, 2024, inahusiana na uhalali wa kifungu cha 178, 243, 244, 245, 246, 247, 248, 249, 250, 256, 257, na 259 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, Sura ya 20 ambavyo vinaruhusu mtuhumiwa kufunguliwa kesi katika Mahakama za Chini (Committal Proceedings) wakati upelelezi ukiwa haujakamilika kwa makosa ambayo Mahakama Kuu ndiyo ina mamlaka ya kusikiliza kesi hizo.
 
Kwa mujibu wa taarifa ya THRDC, kesi hiyo ilipaswa kusomwa Desemba 10, 2024, lakini ikaahirishwa hadi Desemba 20, 2024, kisha hadi Januari 14, 2025. Hata hivyo, tarehe hiyo pia haikusomwa, na hatimaye ikaahirishwa tena hadi Februari 6, 2025. Februari 18, 2025, uamuzi huo haukusomwa kwa mara ya tano, kwa sababu Jaji hakuwepo mahakamani.
 
“Hairisho hilo la kusomwa kwa uamuzi mdogo ni la tano (05) bila sababu za msingi, jambo hili linasababisha adha na usumbufu mkubwa kwa mawakili wanaosimamia kesi hii kwa kupoteza muda wao mwingi mahakamani kusubiri kusomwa kwa uamuzi mdogo wa mahakama na badala yake wanaambiwa uamuzi hauko tayari au Mhe. Jaji hayupo na uamuzi hausomwi, na kama uamuzi huo ukiwa tayari ungewezwa kusomwa na Msajili au naibu msajili wa Mahakama kuu kama ambavyo sheria inaelekeza”, imeeleza THRDC.
 
THRDC imetoa wito kwa Mheshimiwa Jaji Mkuu wa Tanzania kuhakikisha kuwa maamuzi yote yanatolewa kwa wakati ili kuimarisha imani ya wananchi katika mfumo wa mahakama.
 
“Kucheleweshwa kusomwa kwa wakati kwa maamuzi ya Mahakama katika kesi hii ni kinyume cha Kanuni zinazoongoza mashauri ya kikatiba nchini, ambapo kwa mujibu wa kanuni ya 9 (1) ya Kanuni za Sheria ya Haki Msingi na Wajibu (Mwenendo na Utaratibu) za Mwaka 2014 inaelekeza kwamba Mhe. Jaji anapaswa kutoa uamuzi wa mapingamizi ndani ya siku 30. Katika shauri hili tangu Mhe. Jaji Manyanda apangiwe kusikiliza shauri hili na kupangwa kwa uamuzi mdogo sasa ni zaidi ya siku 30 zinazohitajika kwa mujibu wa sharia”, imeeleza THRDC.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!