Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala ndogo ya Dar es Salaam kupitia Jaji Wilfred Ndyansobera imekubaliana na hoja zilizowasilishwa na wananchi watatu (3) ambao ni Bob Chacha Wangwe, Bubelwa Kaiza na Dkt. Ananilea Nkya ambapo sasa imetoa kibali cha kuruhusu TAMISEMI kushtakiwa na kupingwa kusimamia uchaguzi wa serikali za mitaa,
Kwa maamuzi hayo sasa ni rasmi kesi ya msingi ya kupinga TAMISEMI kusimamia uchaguzi wa serikali za mitaa itafunguliwa Mahakamani hapo, baada ya Mahakama kubaini kuwa hoja za wajibu maombi (serikali) hazina mashiko kwa sababu maombi hayo yameletwa kwa njia sahihi, na sasa kesi ya msingi inaweza kufunguliwa,
Katika mapingamizi manne yaliyowasilishwa na wajibu maombi (serikali) Mahakamani hapo, Mahakama imetupilia mbali mapingamizi mawili ya awali, imekubaliana na pingamizi la tatu, lakini pia imetupilia mbali pingamizi la nne kwa kuwa nalo halina msingi, hivyo Mahakama kuona kwamba mapingamizi yote ya awali hayana msingi kwa kuwa yamelenga hitaji moja.
Katika sehemu ya hoja zake Mahakama imesema mamlaka inayolalamikiwa ni ya umma (yaani Waziri na Mwanasheria Mkuu wa Serikali) lakini pia wanaolalamika ni wananchi kwa niaba ya umma
Hata hivyo Mahakama hiyo haijakubaliana na hoja ya kusitisha kwa utekelezaji wa sheria ndogo zinazompa mamlaka Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kuratibu uchaguzi wa serikali za mitaa, hivyo TAMISEMI itaendelea kuratibu zoezi la uchaguzi wakati kesi ya msingi itakayofunguliwa inaendelea, isipokuwa kwa sasa waleta maombi wanaweza kufungua rasmi jambo hilo upya kwa kuwa isingewezekana Mahakama kusitisha zoezi linaloendelea wakati kibali hakijatoka.