Latest Posts

MAHAKAMA YASITISHA AMRI YA TRUMP YA KUZUIA URAIA WA KUZALIWA MAREKANI

Jaji wa Mahakama ya Wilaya ya Marekani, John Coughenour, ametoa agizo la muda la kusitisha utekelezaji wa amri ya Rais Donald Trump ya kufuta uraia wa kuzaliwa nchini Marekani.

Amri hiyo, iliyolenga kuwanyima watoto wa wahamiaji wasio na nyaraka au walio na visa za muda haki ya uraia, ilipingwa vikali na majimbo manne ya Marekani: Washington, Arizona, Illinois, na Oregon.

Jaji Coughenour amehitimisha kuwa amri hiyo ya Trump ni kinyume cha Katiba, haswa dhidi ya Marekebisho ya 14 ya Katiba ya Marekani, ambayo inatamka wazi kuwa “watu wote waliozaliwa au waliopata uraia ndani ya Marekani, na wanaoshughulikiwa na mamlaka yake, ni raia wa Marekani.”

Majimbo yaliyopinga amri hiyo yalieleza kuwa utekelezaji wake ungeathiri vibaya maelfu ya raia wa Marekani na familia zao. Kulikuwa na ripoti kwamba utawala wa Trump ulikuwa unapanga kudhibiti nyaraka muhimu, kama pasipoti, kutoka kwa watu waliodhaniwa kuwa hawastahili uraia.

Katika maamuzi yake, Jaji Coughenour alitoa agizo la muda la kusitisha utekelezaji wa amri hiyo kwa siku 14, akisema suala hilo linahitaji kusikilizwa zaidi. Mawakili wa serikali kuu, kwa upande wao, wameahidi kukata rufaa na wameeleza kuwa kesi hiyo huenda ikafikishwa mbele ya Mahakama Kuu ya Marekani.

Marekebisho ya 14 ya Katiba ya Marekani, yaliyopitishwa mwaka 1868, yamekuwa msingi wa uraia wa kuzaliwa kwa wote waliyozaliwa kwenye ardhi ya Marekani. Marekebisho haya yamefasiriwa na mahakama kama kutoa haki ya uraia bila kujali hadhi ya kisheria ya wazazi wa mtoto.

Kwa mujibu wa takwimu za kisheria, zaidi ya watoto 255,000 walizaliwa nchini Marekani mnamo 2022 na mama wasio na nyaraka. Trump alikusudia kubadilisha tafsiri ya sheria hii, lakini mabadiliko kama haya yanahitaji sheria mpya au uamuzi wa Mahakama Kuu, jambo ambalo ni gumu kisheria.

Mpango wa Trump umekuwa ukizua mijadala mikali kuhusu haki za wahamiaji na usawa wa kikatiba. Wakosoaji wake wanasema kuwa juhudi za kubadilisha sheria za uraia ni sehemu ya ajenda pana ya kupunguza wahamiaji, huku wafuasi wake wakihimiza sera kali za uhamiaji kwa misingi ya usalama wa taifa.

Rufaa inayotarajiwa kutoka kwa mawakili wa serikali inaonesha kuwa suala hili halijaisha, na kuna uwezekano mkubwa wa kesi hii kuathiri tafsiri za kikatiba kwa muda mrefu.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!