Rais wa Marekani Donald Trump ametangaza kusitisha kwa muda ushuru wa asilimia 25 kwa bidhaa kutoka Mexico na Canada kwa kipindi cha mwezi mmoja, kufuatia mazungumzo yake na Rais wa Mexico, Claudia Sheinbaum, na Waziri Mkuu wa Canada, Justin Trudeau.
Baada ya mazungumzo hayo, Rais Sheinbaum alitangaza kuwa Mexico itatuma wanajeshi 10,000 kwenye mpaka wake wa kaskazini ili kudhibiti ulanguzi wa dawa za kulevya, hususan fentanyl, kuelekea Marekani.
“Mexico itaweka doria kwenye mpaka wa kaskazini ili kuzuia ulanguzi wa dawa kutoka Mexico, hasa fentanyl,” aliandika kupitia mtandao wa X. Sheinbaum pia alisema kuwa Marekani imeahidi kusitisha upelekaji wa silaha haramu kwenda Mexico.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Canada, Justin Trudeau, alisema kuwa Canada itatumia teknolojia mpya pamoja na kuongeza wafanyakazi kwenye mpaka wake na Marekani ili kudhibiti usafirishaji wa fentanyl.
Ikulu ya Marekani (White House) haijatoa tamko rasmi kuhusu makubaliano hayo, lakini Trump aliwaambia wanahabari kuwa mazungumzo yake na Trudeau yalikuwa mazuri.
Kwa sasa, mataifa yote matatu yataendelea kushirikiana katika masuala ya usalama na biashara, huku ushuru uliotangazwa awali ukisitishwa kwa mwezi mmoja wakati hatua zaidi zikifanyiwa tathmini.