Latest Posts

MIRADI YA MAJI YENYE THAMANI YA BILIONI 32 YABORESHA HUDUMA KATAVI

Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko, amesema kuwa katika kipindi cha uongozi wa Rais wa Awamu ya Sita, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, mkoa huo umeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo, ukiwemo utekelezaji wa miradi mitano mikubwa ya usambazaji maji yenye thamani ya Shilingi bilioni 32,163,080,399.89 Mradi huu unatarajiwa kuongeza upatikanaji wa huduma ya maji kwa zaidi ya asilimia 100 baada ya kukamilika.

Mrindoko alitoa kauli hiyo jijini Dodoma alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita katika mkoa wa Katavi.

Ameeleza kuwa Mkoa unaendelea kutekeleza mradi wa usambazaji maji kutoka Bwawa la Milala, unaotekelezwa chini ya mpango wa ujenzi wa miradi ya maji kwa miji 28 nchini. Mradi huo unatarajiwa kuzalisha lita milioni 12 za maji kwa siku na utanufaisha wakazi wote wa Manispaa ya Mpanda.

“Hadi kufikia Juni 2025, utekelezaji wa mradi huu umefikia asilimia 42. Unatekelezwa kwa kipindi cha miezi 30 kuanzia Aprili 11, 2023, na unatarajiwa kukamilika mwezi Oktoba 2025,” amesema Mrindoko.

Kwa upande wa huduma ya maji vijijini, amesema kuwa katika kipindi cha uongozi wa Rais Dkt. Samia, mkoa umepokea Shilingi bilioni 33.53 kupitia Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kwa ajili ya kutekeleza miradi 51 ya maji.

“Utekelezaji wa miradi hiyo umeongeza uwiano wa watumiaji wa maji vijijini kutoka asilimia 62.2 mwaka 2021 hadi asilimia 77.3 ifikapo Juni 2025, sawa na ongezeko la asilimia 15.1 “.

Aidha, Mrindoko amesema kuwa mkoa umepokea Shilingi bilioni 196.4 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya nishati, ikiwemo upanuzi wa mtandao wa umeme na kuboresha nguvu ya umeme (voltage improvement) katika wilaya za Mpanda, Tanganyika na Mlele.

“Kwa ufadhili wa REA awamu ya kwanza, vijiji vyote 172 vya mkoa wa Katavi vimeunganishiwa umeme. Hadi Juni 2025, jumla ya vitongoji 504 kati ya 912 vitakuwa vimepata umeme, huku vitongoji 408 vilivyosalia vikitarajiwa kuunganishwa katika bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026,” amesema.

Ameongeza kuwa huduma hizo zimeongeza idadi ya wateja wa umeme kutoka 23,312 mwaka 2020/21 hadi 42,567 kufikia Juni 2025. Ongezeko hilo pia limechochea mapato kutoka Shilingi milioni 494.5 hadi Shilingi bilioni 1.03 kwa mwezi.

Mbali na hayo, Mkuu huyo wa Mkoa amepongeza juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuleta Shilingi trilioni 0.41 (410,975,698,026.00) kwa ajili ya miradi ya kimkakati na ya kitaifa.

“Miradi hii itakapokamilika, mtandao wa barabara za kiwango cha lami utaongezeka kutoka kilomita 325.81 hadi kufikia kilomita 548.45,” ameeleza Mrindoko.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!