Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) ambaye pia ni Jaji wa Rufaa Jacobs Mwambegele amesema zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura mkoani Morogoro unatarajia kuanza Machi 01 hadi 07 mwaka huu ili kutoa fursa kwa watanzania wengi kushiriki uchaguzi mkuu utakaofanyika Novemba, 2025.
Jaji Mwambegele amethibitisha hayo mkoani Morogoro katika mkutano wa Tume na wadau wa uchaguzi kuhusu uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura Mkoa wa Morogoro.
Amesema Tume hiyo imeanza maandalizi ya uboreshaji wa daftari la mpiga kura ambapo katika zoezi hilo itahusisha matumizi ya mifumo ya kielektroniki (BVR) ili kurahisisha uboreshaji huo na kuhifadhiwa kwenye kanzidata ya wapiga kura.
“Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa, Tume imeanza maandalizi ya mzunguko wa 12 kati ya mizunguko 13 ya uboreshaji wa daftari,mzunguko huu wa 12 unahusisha Mkoa huu wa Morogoro” amesema Jaji Mwambegele.
Amesema, Tume hiyo imekamilisha zoezi hilo katika mikoa 27 ikiwemo Kigoma, Tabora, Katavi, Geita, Kagera, Mwanza, Shinyanga, Mara, Simiyu, Manyara, Dodoma na Singida. Mikoa mingine ni Mjini Magharibi, Kusini Unguja, Kaskazini Unguja, Kusini Pemba, Kaskazini Pemba, Arusha, Kilimanjaro, Mbeya, Iringa, Rukwa, Songwe, Njombe, Ruvuma, Lindi na Mtwara.
Kwa sababu hiyo, Jaji Mwambegele amewasisitiza wadau mbalimbali kuhamasisha wananchi na kutoa elimu ili kujitokeza kwa wingi kujiandikisha, na kuboresha taarifa zao huku akiwataka wazee, watu wenye ulemavu, wagonjwa, wajawazito na akina mama wenye watoto wachanga watapewa kipaumbele.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Uchaguzi hapa nchini (INEC) Ramadhani Kailima amesema mkoani Morogoro, Tume inatarajia kuandikisha wapiga kura wapya 302,752 sawa na ongezeko la asilimia 18.7 ya wapiga kura 1,612,952 waliokuwepo kwenye daftari la wapiga kura mwaka 2020.