Moto mkubwa uliozuka katika hoteli ya ghorofa 12 kwenye kituo maarufu cha michezo ya kuteleza huko kaskazini magharibi mwa Uturuki umeua watu wasiopungua 66 na kuwajeruhi wengine 51, kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uturuki, Ali Yerlikaya.
Kwa mujibu wa Citizen Digital, moto huo ulitokea katika hoteli ya Grand Kartal, iliyopo kwenye kituo cha Kartalkaya katika milima ya Koroglu, jimbo la Bolu, takriban kilomita 300 mashariki mwa Istanbul. Tukio hilo limetokea wakati wa mapumziko ya muhula wa shule, kipindi ambacho hoteli za eneo hilo huwa zimejaa wageni.
Waziri wa Afya, Kemal Memisoglu, amesema kuwa mmoja wa majeruhi yupo katika hali mbaya, huku watu 17 wakiruhusiwa kutoka hospitalini baada ya kutibiwa. Hoteli hiyo ilikuwa na wageni 238 waliosajiliwa wakati moto ulipotokea. Moto uliripotiwa saa 9:27 alfajiri na kikosi cha zima moto kilianza kufika eneo hilo saa 10:15 alfajiri.
Gavana Abdulaziz Aydin alisema kuwa waathirika wawili walifariki baada ya kuruka kutoka kwenye jengo kwa hofu, huku wengine wakijaribu kushuka kutoka kwenye vyumba vyao kwa kutumia mashuka na mablanketi.
Necmi Kepcetutan, mwalimu wa mchezo wa kuteleza katika hoteli hiyo, amesema kuwa alikuwa amelala wakati moto ulipoanza na alikimbilia nje ya jengo mara moja. Alisaidia wageni 20 kutoka nje salama. “Sikuweza kufika kwa baadhi ya wanafunzi wangu. Natumaini wako salama,” alisema kwa wasiwasi.
Atakan Yelkovan, mgeni aliyekuwa akikaa kwenye ghorofa ya tatu, alisema mke wake alihisi harufu ya moto lakini kengele ya tahadhari haikumuamsha. “Tulijaribu kupanda juu, lakini moto ulikuwa umeenea. Tukashuka chini na kutoka nje,” alieleza.
Taratibu za uzimaji moto zilikabiliwa na changamoto nyingi kutokana na eneo la hoteli hiyo, ambapo sehemu ya hoteli iko kwenye ukingo wa mwamba. “Kwa sababu upande wa nyuma uko kwenye mteremko, hatua za kuzima moto ziliwezekana tu kutoka mbele na pembeni,” alisema Yerlikaya.
Ripoti za vyombo vya habari zilieleza kuwa mbao zilizotumika kutengeneza hoteli hiyo zilichangia kuenea haraka kwa moto.
Serikali imeteua waendesha mashtaka sita kuongoza uchunguzi kuhusu chanzo cha moto, ambao unahisiwa kuanzia kwenye sehemu ya mgahawa wa hoteli. Rais Recep Tayyip Erdogan amesema: “Tutachukua hatua zote muhimu kufichua ukweli wa tukio hili na kuwawajibisha wahusika.”
Hoteli hiyo ilikuwa imekaguliwa mara ya mwisho mwaka 2024, na hakukuwa na ripoti ya kasoro yoyote kuhusiana na uwezo wa kukabiliana na moto, kulingana na Waziri wa Utalii, Mehmet Nuri Ersoy.