Latest Posts

MPINA AGONGA MWAMBA MAHAKAMANI, KESI YA SPIKA

Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala ndogo ya Dar es Salaam , Alhamisi Oktoba 24.2024 imekubaliana na mapingamizi mawili (2) yaliyokuwa yamewekwa na Jamhuri kwenye kesi iliyokuwa imefunguliwa na Mbunge wa jimbo la Kisesa (CCM) Luhaga Mpina dhidi ya Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Waziri wa Kilimo na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) hivyo Mahakama kutupilia mbali shauri hilo
Katika maelezo yake Mahakama hiyo imesema haina mamlaka ya kuingilia maamuzi yaliyofanywa ndani ya kuta nne za Bunge ikizingatiwa muongozo wa mgawanyo wa mamlaka kati ya muhimili mmoja na mwingine, sambamba na hilo Mahakama imerejea uamuzi iliyokuwa imeutia miaka ya nyuma kati ya Augustine Mrema  dhidi ya Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa  Tanzania ambapo maamuzi kama hayo yalifanyika
Itakumbukwa kuwa katika shauri la msingi Mbunge Luhaga Mpina alikuwa anapinga mchakato uliotumika kumuondoa Bungeni (kuzuiwa kuhudhuria vikao 15 vya Bunge), akidai kuwa mchakato huo ulienda kinyume na misingi ya Kanuni za Kudumu za Bunge, sheria na taratibu za nchi jambo ambalo Mahakama imesema haiwezi kuingilia maamuzi hayo kwa kuheshimu mgawanyo wa madaraka
Akizungumza na wanahabari kwenye viunga vya Mahakama hiyo Mbunge Mpina amesema hakubaliani na maamuzi hayo hivyo haraka iwezekanavyo amewaelekeza Mawakili wake kukata rufaa Mahakama ya rufani ili kupinga maamuzi hayo
Katika kesi hiyo Mpina alikuwa anawakilishwa na jopo la Mawakili waliokuwa wanaongozwa na Mpare Mpoki, akishirikiana na Dkt. Rugemeleza Nshala, John Seka, Boniface Mwabukusi, Ferdinand Makore, Edson Kilatu nk,
Kwa upande wa wajibu maombi (yaani Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Waziri wa Kilimo na Mwanasheria Mkuu wa Serikali) katika shauri hilo walikuwa wanawakilishaa na Wakili wa Serikali Mkuu, Hangi Chang’a akishirikiana na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Pauline Mdendemi na wengineo
Katika hatua nyingine Mahakama hiyo imesema kwenye kesi hiyo hakukuwa na ulazima wa kujumlishwa kwa Waziri wa Kilimo
Kufuatia hatua hiyo, kwa sasa Mpina amesaliwa na kesi moja kwenye Mahakama hiyo ambayo ni ile aliyoifungua dhidi ya Waziri wa Kilimo, Waziri wa Fedha, Kamishna Mkuu wa TRA, Bodi ya Sukari, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na baadhi ya makampuni binafsi, ambapo katika kesi hiyo Mpina anapinga utaratibu uliotumika na serikali kutoa vibali vya kuagiza Sukari kutoka nje ya nchi
Sambamba na hilo kwenye Mahakama hiyo pia ipo kesi iliyofunguliwa na wakulima wa miwa wa Bonde la Kilombero dhidi ya Waziri wa Kilimo, Waziri wa Fedha, Bodi ya Sukari na Mwanasheria Mkuu wa Serikali,
Jambo TV itakuletea taarifa zaidi kuhusu maamuzi hayo

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!