News, Njombe.
Watumishi wa Afya halmashauri ya mji wa Njombe wametakiwa kutowatoza fedha wagonjwa kwa ajili ya kulipia gari la kubebea wagonjwa kwani tayari Serikali imeshagharamia hivyo wagonjwa wanatakiwa kubebwa bure.
Kauli hiyo imetolewa Januari 8, 2025 na Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji wa Njombe Jabir Juma wakati wa hafla ya kukabidhi gari la kubeba wagonjwa katika kituo cha afya cha Ihalula kilichopo kata ya Utalingolo Halmashauri ya Mji wa Njombe.
Amesema isijekutokea wananchi wakalalamika kuhusu kutozwa fedha kwa ajili ya gharama za kusafirisha wagonjwa kutoka sehemu moja kwenda nyingine kwa ajili ya kupata matibabu wakati serikali imetoa gari hilo bure ili kuboresha huduma kwa wananchi.
“Tusije tukaanza kulalamika watumishi hatufanani inawezekana siku moja akaingia tamaa au kushawishika na kuomba hela ya mafuta atakuwa ameteleza lakini mwananchi jua usafiri ni bure”, amesema Juma.
Mbunge wa Njombe Mjini Deo Mwanyika amesema zaidi ya bilioni mbili zimetengwa ili kujenga vituo vya Afya katika Halmashauri ya mji wa Njombe na lengo ni kupunguza changamoto za kukosekana kwa huduma za afya kwa wananchi.
“Tumejenga vituo vitano vya afya katika vituo hivyo vinne vimejengwa kwa mapato ya ndani ya Halmashauri ya mji wa Njombe na kituo kimoja cha Luponde kinajengwa kwa fedha za serikali za tozo”, amesema Mwanyika.
Diwani wa kata ya Utalingolo, Erasto Mpete ambaye pia ni mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Njombe Erasto Mpete amewataka wananchi kulitunza gari hilo ili liwasaidie pamoja na vizazi vijavyo.