Imeelezwa kuwa ni asilimia saba pekee ya Watanzania wanaotumia kahawa inayozalishwa nchini, huku asilimia 93 ikiuzwa nje ikiwa katika mfumo wa clean coffee hali inayolenga Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB) kuongeza matumizi ya ndani hadi asilimia 15 ili kukuza soko na kuongeza thamani ya zao hilo.
Mkurugenzi wa Masoko wa TCB, Frank Nyarusi, amesema mkakati huo unatekelezwa kwa kushirikiana na wadau kupitia mwezi maalumu wa uhamasishaji kuhusu matumizi, ubunifu, uzalishaji na ubora wa kahawa. “Zao la kahawa ni zao bunifu, kila wakati kuna jambo jipya la kibunifu linaloweza kufanyika katika jamii,” amesema Nyarusi.
Nyarusi ameyasema hayo mjini Moshi wakati wa uzinduzi wa Msimu wa Saba wa Kahawa Festival, akisisitiza kuwa kahawa si zao la kilimo pekee, bali pia ni fursa ya ubunifu na ujasiriamali. Amesema vijana na wafanyabiashara wanaweza kutumia kahawa kutengeneza bidhaa na huduma zenye kuongeza thamani.

Kwa upande wa uzalishaji, TCB imeeleza kuwa kahawa imeongezeka kutoka wastani wa tani 50,000 hadi kati ya tani 80,000 na 100,000 kwa sasa.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Kahawa Festival, Denis Mahulu, amesema uzalishaji wa miche unalengwa kuongezeka kutoka 20,000 hadi 30,000 katika msimu wa 2026/27.
Akizindua tamasha hilo, Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mnzava, amewataka wadau kuzingatia ubora, uendelevu na viwango vya masoko. “Matumizi ya teknolojia yanaweza kuwa nyenzo muhimu katika kuwafikia walaji na wanunuzi wa kahawa ndani na nje ya nchi,” amesema Mnzava.
Mkakati wa kuongeza matumizi ya ndani kutoka asilimia saba hadi 15 unalenga kujenga soko la ndani, kuongeza fursa za biashara na kuhakikisha thamani zaidi ya kahawa inabaki nchini na kuwanufaisha wakulima, vijana na wafanyabiashara.
Msimu wa Saba wa Kahawa Festival umebeba kaulimbiu “Kahawa Ni Sehemu ya Suluhisho, Kujenga Ustawi Kupitia Mashindano.”