Rais wa Uganda, Yoweri Kaguta Museveni, mwenye umri wa miaka 80, ametangaza nia ya kuwania muhula wa saba katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Januari mwaka ujao
Kupitia chapisho katika ukurasa wake wa X (zamani Twitter), Museveni alisema ameonesha dhamira ya kugombea nafasi ya mshika bendera wa urais kwa tiketi ya chama tawala, na kueleza matumaini yake ya kuifikisha Uganda kwenye uchumi wa thamani ya dola bilioni 500 ndani ya miaka mitano ijayo.
Iwapo atachaguliwa tena, Museveni anaweza kuongoza taifa hilo kwa karibu nusu karne, tangu aliponyakua madaraka mwaka 1986 baada ya mapinduzi ya kivita.
Tangu wakati huo, katiba ya nchi hiyo imefanyiwa marekebisho mara mbili—ikiondoa kikomo cha mihula na kisha cha umri wa kugombea urais—hili likiwa ni miongoni mwa sababu zinazozua ukosoaji kutoka kwa vyama vya upinzani na wanaharakati wa haki za binadamu
Wapinzani wake, akiwemo mwanamuziki aliyegeuka kuwa mwanasiasa Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine, wametangaza tena nia ya kushindana naye. Bobi Wine alishika nafasi ya pili katika uchaguzi wa 2021, lakini alikataa matokeo hayo, akidai yaligubikwa na wizi wa kura, madai yaliyokanushwa na serikali na tume ya uchaguzi.
Bobi Wine ameendelea kuikosoa serikali ya Museveni kwa madai ya ukiukaji wa haki za binadamu, mateso, utekaji na kizuizi kinyume cha sheria dhidi ya wapinzani wake. Ameitaka jumuiya ya kimataifa kutoangalia pembeni hali hiyo, akihimiza kuwajibika kwa haki na demokrasia.
Tume ya Uchaguzi ya Uganda imetangaza kuwa uchaguzi mkuu wa rais utafanyika Januari 2026.