Na Amani Hamisi Mjege.
Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Wakili Boniface Mwabukusi, ameonesha masikitiko juu ya jinsi ambavyo jeshi la polisi linavyoshughulikia maandamano na mikutano ya kisiasa nchini.
Akizungumza katika mahojiano na Jambo TV, Mwabukusi ameeleza kuwa sheria ya vyama vya siasa inatoa haki kwa chama cha siasa kufanya maandamano au mikutano, lakini utekelezaji wa sheria hiyo umekuwa na changamoto kutoka kwa jeshi la polisi.
Mwabukusi amebainisha kuwa polisi wamekosa kufuata taratibu zinazotakiwa kisheria katika barua zao za kuzuia mikutano ya kisiasa.
“Upande wa polisi, changamoto niliyoiona ni kwamba hawakujielekeza vizuri katika masharti ya sheria. Barua yao haikueleza ipasavyo sababu za kisheria za kuzuia maandamano hayo,” alisema Mwabukusi.
Ameongeza kuwa, kwa mujibu wa sheria ya vyama vya siasa, polisi hawana mamlaka ya kupima uhalali wa shughuli za kisiasa bali msajili wa vyama vya siasa ndiye mwenye mamlaka hiyo.
“Ni msajili wa vyama vya siasa pekee anayepaswa kueleza kama kuna dosari kwenye maandamano au mikutano,” alisisitiza Mwabukusi.
Katika hatua nyingine, Mwabukusi ameeleza kwa kina kuwa maandamano siyo uhalifu bali ni haki ya kikatiba ambayo imetajwa katika sheria ya vyama vya siasa. Amewataka wale wanaodhani kuwa maandamano ni uhalifu kuleta hoja za kuyaharamisha kisheria, badala ya kulinganisha maandamano na ghasia.
“Maandamano ni njia bora ya kuonyesha hisia, siyo uhalifu. Ndiyo maana kwenye sheria ya vyama vya siasa, inatambuliwa kama haki ya chama kufanya maandamano,” alisema.
Akizungumzia msimamo wa TLS kuhusu hali ya kisiasa na maandamano nchini, Mwabukusi ameeleza kuwa chama chake hakipingani na maandamano, bali kimeamua kuandaa kongamano litakalojumuisha wadau mbalimbali kujadili suala hilo.
“Sisi TLS hatupingi chochote, tunaandaa kongamano kwa ajili ya wanataaluma, mashirika ya kijamii, na viongozi wa umma ili tujadiliane kwa pamoja,” amesema.
Mwabukusi amewahimiza viongozi wa kisiasa kuacha lawama na badala yake watafute majadiliano ya pamoja kwa ajili ya kutatua changamoto zinazolikumba taifa. Amekubaliana na kauli ya Katibu Mkuu wa CCM Dkt. Emmanuel Nchimbi kuwa kuna changamoto katika sekta ya kisiasa na akataka viongozi wakubali kukaa mezani na kujadili suluhisho.
“Tuache kunyoosheana vidole, tukae na serikali, CHADEMA walikuwa na haki ya kutumia njia waliyotumia lakini hili jambo linahitaji zaidi ya majadiliano,” ameongeza Mwabukusi.